Tanzania imeendelea kung’ara kimataifa katika sekta ya utalii baada ya kuteuliwa kuwa mwenyeji wa hafla kubwa ya kimataifa ya utoaji wa Tuzo za Utalii za World Travel kwa kanda ya Afrika na Bahari ya Hindi, itakayofanyika Juni 28, 2025 jijini Dar es Salaam.
Tukio hili linaloratibiwa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), linatajwa kuwa uthibitisho wa nafasi ya Tanzania kama kinara wa sekta ya utalii barani Afrika, na ni hatua nyingine kubwa inayotokana na juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kutangaza vivutio vya nchi kupitia kampeni ya Royal Tour.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 14, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii, Ephraim Mafuru, alisema tuzo hizo zilizozinduliwa mwaka 1993 na Kampuni ya World Luxury Media Group, ni jukwaa linalotambua na kusherehekea mafanikio ya watoa huduma wa utalii duniani.
“Uteuzi wa Tanzania kuwa mwenyeji wa hafla hii ya heshima kubwa ni matokeo ya kazi kubwa ya kutangaza vivutio vyetu. Ni fursa ya kipekee kwa nchi kuonesha uwezo wake na kuhamasisha wawekezaji na watalii kutoka duniani kote,” alisema Mafuru.
Akitaja mafanikio zaidi, Mafuru alisema Tanzania imeteuliwa kushindania zaidi ya vipengele 15 vya tuzo hizo, ikiwemo:
*Nchi inayoongoza kwa Utalii Afrika
*Bodi Bora ya Utalii (TTB)
*Kivutio Bora cha Utalii (Ngorongoro)
*Mlima Bora Afrika (Kilimanjaro)
*Hifadhi Bora Afrika (Serengeti)
*Uwanja Bora wa Ndege (JNI
*Bandari Bora (Dar es Salaam)
*Fukwe bora za Zanzibar
Aidha, aliwahimiza Watanzania kushiriki kwa kupiga kura kuunga mkono vivutio vya nyumbani na kuhakikisha Tanzania inaibuka na ushindi, huku akibainisha kuwa zaidi ya nchi 30 zitashiriki tukio hilo, zikiwemo kampuni za kimataifa, wawekezaji, waandishi wa habari na wadau wa utalii.
“Hili ni jukwaa la kuimarisha nafasi ya Tanzania katika ramani ya utalii duniani. Tuitumie fursa hii kuonesha ubora wetu na kupokea wageni kwa ukarimu,” alisisitiza.