Waziri Dkt. Ndubaro amesema kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka bayana sababu zinazoweza kusababisha Mtanzania kutoshiriki uchaguzi na imebainisha uchaguzi kama haki ya Msingi ya Kila mwananchi mwenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea, hivyo kumzuia kushiriki ni kumnyima haki yake ya kibinadamu.
Waziri Huyo wa Katiba na Sheria Dkt. Ndumbaro aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa kampeini ya kisheria katika mkoa wa Kagera iliyofanyika katika viwanja vya Mayunga vilivyopo Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, ambapo mamia ya wananchi wamejitokeza kuleta changamoto zao za kisheria na kuziwasilisha kwa wanasheria huku wengine wakipata Fursa ya kukabidhiwa mawakili mbele ya Waziri huyo.
Kupitia Kampeini hiyo amewahakikishia wakazi wa mkoa wa Kagera kuwa kampeini hiyo ni endelevu na tayari wizara imewaajili maafisa Dawati wa kushughulikia malalamiko ya kisheria wilayani wapatao 400 nchi nzima, huku wanasheria wasaidiz waliopewa mafunzo kwa ajili ya kutoa huduma za kisheria wamefikia 2,500.
“Wananchi msiwe na wasiwasi tumeshuhudia mafanikio makubwa sana kupitia kampeini ya mama Samia ya msaada wa kisheria na toka kampeni hii ianzishwe mwaka 2023 Asasi za kiraia zinazotoa huduma za kisheria zimeongezeka kutoka 85 Hadi 387″alisema Ndumbalo.
Alitoa wito kwa viongozi wa Dini kutoacha kukemea wananchi wanaojichukulia Sheria mkononi, kwani wanageuka chanzo cha mitafaruku na migogoro iisiyoisha ,pia amezitaka familia kutafuta suluhisho la kupatana kwani familia nyingi ndizo chimbuko la migogoro ya Ardhi na Miradhi.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Kagera Mhe. Fatma Mwassa alisema kuwa, mkoa huo utawavua mamlaka Wenyeviti wa vijiji na Mitaa pamoja na kuwatengua watendaji wa mitaa na vijiji wanaosababisha migogoro ya Ardhi kwani wao wamekuwa chanzo cha migogoro ya Ardhi mara kwa mara
“Mkoa wa Kagera huu hata vitendo vya mauaji mara nyingi vinasababishwa na migogoro ya Ardhi ,mara nyingi wenyeviti wa vijiji wanauza maeneo ya wananchi migogoro haiishi na hapohapo tunapata watu wanalipiza visasi ,sasa kama mkoa tunapanga kuchukua hatua madhubuti ,kuwawajibisha”alisema Mwassa
Aidha ameipongeza Mahakama kuu Kanda ya Bukoba na Mahakama ya Hakimu mfawithi wilaya ya Bukoba kwa jinsi wanavyoendelea kupambana na kesi za ukatili wa Kijinsia na kuhakikisha kuwa watuhumiwa wa vitendo vya ubakaji na ulawiti wanavyowajibishwa kisheria .