Na WMJJWMM, Tarime – Mara
Wataalam mbalimbali wa Ngazi ya Kata kutoka katika Halmashauri za Wilaya ya Tarime wametakiwa kujitambua kuwa wao ndio watatuzi wa kwanza wa kero na changamoto zozote za kukwamisha maendeleo zitakazojitokeza katika mazingira yao.
Hayo yamesemwa Aprili 14, 2025 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Felister Mdemu wakati akifungua mafunzo ya mageuzi ya kifikra na mtazamo wa kuwafanya wananchi kuwa kitovu cha maendeleo katika Kampeni ya Amsha Ari inayoendelea kutekelezwa mkoani Mara.
Felister amefafanua kuwa Serikali imeweka nguvu na kuwaajiri wataalam wengi ili waweze kuwasaidia wananchi kuanzia ngazi ya msingi hivyo ni wajibu kila mmoja kufanya kazi kwa juhudi, kujituma na kuifurahia nafasi hiyo.
“Twendeni tukatekeleze majukumu yetu vyema huku tukiamiamini kuwa jukumu hili ni letu na sio kusubiria viongozi ngazi ya taifa wafike na kubaini changamoto za wananchi wakati sisi tumepewa nafasi hii ya kuwahudumia wananchi” amesema Felister.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Patrick Golwike akitoa mada ya kuhamasisha na kusimamia Maendeleo Ngazi ya Jamii amewataka wataalam hao kwenda kutoa kicheko kwa kutoa elimu na kuwahudumia wananchi na sio vinginevyo.
“Twende tukawape kicheko wananchi tunaowahudumia kwa kufurahia huduma tunazozifanya kwa kutatua changamoto zilizopo na kuleta suluhu za changamoto hizo” ameeleza Patrick
Mafunzo haya yametolewa kwa wataalam ngazi ya Kata kutoka katika Halmashauri za Wilaya ya Tarime wakiwa ni Maafisa Maendeleo ya Jamii, Maafisa Kilimo na Mifugo, Watendaji wa Kata, Wataalam wa Dawati la Jinsia toka Jeshi la Polisi, wlWataalam wa Afya ya Jamii ambao kwa pamoja ni sehemu ya utekelezwaji wa Kampeni ya Amsha Ari inayoendelea mkoani Mara.