Na; Mwandishi Wetu – Dodoma
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amesema serikali kupitia ofisi hiyo imepanga kwa Mwaka wa fedha 2025/26 kutoa Sh. Milioni 637 zitakazowasaidia vijana wanaofuzu mafunzo ya uanagenzi kupewa vitendea kazi.
Mhe. Katambi amesema hayo wakati akichangia hoja za Wabunge mbalimbali leo Aprili 15, 2025 bungeni kuhusu bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa fedha 2025/26.
Aidha, Mhe. Katambi amesema serikali imetoa zaidi ya Sh.Bilioni moja kwa ajili ya vitendea kazi kwa vijana 1,977 wanaomaliza mafunzo ya uanagenzi na vikundi vya vijana zaidi ya 2700 vimenufaika.
Akizungumzia suala la ajira, Naibu Waziri Katambi amefafanua kuwa ajira zimeendelea kutolewa katika sekta ya umma na binafsi na kwamba maagizo ya Rais Samia na maelekezo ya kiutekelezaji ya Waziri Mkuu ya kila Wizara za kisekta yamewezesha kuzalishwa ajira 8,084,000.
Amebainisha kuwa serikali itaingia mikataba na nchi nane ili vijana wa kitanzania wanufaike na fursa za ajira nje ya nchi na tayari vijana zaidi ya 500 wamenufaika awamu ya kwanza.
Mhe. Katambi amempongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kiongozi shupavu, makini na ameonesha busara kubwa katika maamuzi yake yanayowezesha tija katika sekta ya Ajira, Ukuzaji Ujuzi na Maendeleo ya Vijana.