Na Silivia Amandius
Kagera
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro, amewataka Watanzania kupuuza kauli za wanasiasa wanaozunguka maeneo mbalimbali nchini wakieneza taarifa za uchochezi kuhusu Uchaguzi Mkuu, akisisitiza kuwa uchaguzi ni haki ya msingi ya kila Mtanzania mwenye umri wa kuanzia miaka 18 kama ilivyoelezwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dk. Ndumbaro alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya msaada wa kisheria iliyofanyika katika viwanja vya Mayunga, Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera. Mamia ya wananchi walihudhuria tukio hilo, wakipata fursa ya kuwasilisha changamoto zao za kisheria kwa wanasheria waliopo na wengine kupewa mawakili kwa msaada wa kisheria.
Amesema kuwa kampeni hiyo ni endelevu na tayari wizara yake imeajiri maofisa wa dawati la kisheria wapatao 400 waliotawanywa nchi nzima, huku wanasheria wasaidizi waliopatiwa mafunzo kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria wakifikia 2,500.
“Wananchi msiwe na wasiwasi. Tumeona mafanikio makubwa kupitia kampeni ya Mama Samia ya msaada wa kisheria. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023, idadi ya asasi za kiraia zinazotoa huduma za kisheria imeongezeka kutoka 85 hadi 387,” alisema Dk. Ndumbaro.
Aidha, alitoa wito kwa viongozi wa dini kuendelea kukemea vikali vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi, akibainisha kuwa tabia hiyo ni chanzo cha migogoro isiyokwisha. Vilevile, alizihimiza familia kutafuta suluhu kwa njia ya maelewano kwani migogoro mingi ya ardhi na mirathi hutokea ndani ya familia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, alisema kuwa uongozi wa mkoa huo umejipanga kuwawajibisha viongozi wa vijiji na mitaa wanaochochea migogoro ya ardhi kwa kuwatengua au kuwavua nyadhifa zao.
“Migogoro ya ardhi imekuwa chanzo kikuu cha mauaji katika mkoa wetu. Mara nyingi wenyeviti wa vijiji huuza maeneo ya wananchi bila kufuata utaratibu, jambo linalochochea visasi na uhasama. Kama mkoa, tumeamua kuchukua hatua madhubuti dhidi ya viongozi hao,” alisema Mwassa.