Nyumba ya kuishi familia tatu za walimu wa shule ya msingi Liyombo kata ya Linda Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma inayojengwa na Chama cha Msingi cha Ushirika Liyombo kama inavyoonekana.
Na Mwandishi Wetu, Mbinga
CHANGAMOTO ya nyumba za kuishi walimu katika shule za msingi Liyombo Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma,linakwenda kumalizika baada ya wakulima wa zao la kahawa kupitia Chama cha Msingi cha Ushirika Liyombo Amcos kuanza ujenzi wa nyumba moja ya kuishi familia tatu za walimu wa shule hiyo.
Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Liyombo Amcos Joseph Mbele alisema,wameamua kujenga nyumba hiyo ili kuwanusuru walimu ambao wanaishi mbali ili wawe karibu na maeneo yao ya kazi na kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita kuboresha miundombinu kwenye sekta ya elimu.
Alisema,nyumba hiyo itakapokamilika itasaidia walimu kuwa na makazi bora na ya uhakika hasa ikizingatia kuwa baadhi yao wanaishi uraiani kutokana na upungufu wa nyumba za shule.
Mbele alisema,nyumba wako hatua ya kupiga lipu na tayari wametumia Sh.milioni 17 kati ya Sh.milioni 25 zinazohitaji, lakini changamoto kubwa ni fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo.
Baadhi ya Wakulima wamesema,walimu wakiwa karibu na mazingira ya shule wana uhakika wa kuwahi hususani vipindi vya asubuhi,hivyo kuwawezesha watoto wao kufundishwa mapema na hatimaye kufanya vizuri kwenye masomo darasani.
Dastan Ndunguru,ameipongeza Bodi ya Ushirika Liyombo kwa kazi nzuri inayofanya kuhakikisha wanatumia sehemu ya fedha zinazotokana na ushuru wa kahawa kutekeleza miradi mbalimbali ambayo inachochea maendeleo katika kijiji chao.
Alisema,walimu wa shule ya msingi Liyombo wanaishi kwenye mazingira ambayo siyo rafiki na kuoimba Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya Mbinga kuwaunga mkono ili kukamilisha ujenzi wa nyumba hiyo.
Alisema,kujengwa kwa nyumba hiyo kutawezesha walimu kuishi kwa utulivu na kufanya kazi kwenye mazingira mazuri pamoja na kutekeleza majukumu yao bila kuwa na hofu, jambo litakalosaidia watoto wao kufundishwa vizuri.
“tumeona ni vizuri tuwaweke hawa watu(walimu)karibu na mazingira ya kazi ili wawe wanafundisha watoto wetu kwa ukaribu zaidi,maana watakuwa wanaishi kwenye mazingira haya ya shule hivyo kuwahi kazini”alisema Ndunguru.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Liyombo Emanuel Moshi,ameushukuru uongozi wa Amcos Liyombo kwa kuboresha miundombinu ya shule kwani licha ya kujenga nyumba hiyo imeboresha vyumba vya madarasa ya shule kwa kupiga lipu na kupaka rangi.
Alisema,nyumba hiyo itawasaidia walimu kupata makazi bora hasa ikizingitia kuwa kwa sasa kuna nyumba tatu ambazo ni chakavu na kipindi cha mvua walimu wanapata shida kubwa ya maji kuingia ndani ya nyumba wanazoishi.
Moshi,ameishukuru Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya Mbinga kwa kuwaunga mkono kwa kuwapatia vifaa vya kujifunzia na kufundishi ili waendelee kuwa na mafanikio makubwa katika suala zima la elimu.
Kwa upande wake Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga Nuhu Serenge alisema, Chama cha msingi Liyombo kimefanya mambo mengi na makubwa katika Wilaya ya Mbinga kwa kuchangia maendeleo ya Wilaya hiyo hasa huduma za kijamii.
Alisema, Chama cha Msingi Liyombo kimekuwa Chama cha mfano katika Halmashauri ya Wilaya Mbinga kwa kutoa michango mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Ofisi ya Serikali ya kijiji.
Alisema,michango inayotolewa na Amcos hiyo kwenye jamii ni takwa la kikanuni la Vyama vya Ushirika ambayo ni msingi namba saba na kuwapongeza Wananchi wa kijiji hicho na Ushirika wao kuendelea kuiunga mkono Serikali katika kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.
“Naviomba vyama vingine vya Ushirika katika Halmashauri ya Wilaya Mbinga kuiga mfano mzuri wa Liyombo Amcos, kutoa huduma kwa jamii kwa sababu ni takwa la kikanuni,waisaidie Serikali yetu kuhakikisha huduma hizi zinatekelezwa katika jamii yetu”alisema Serenge.