Na Karama Kenyunko Michuzi Blog
TANZANIA inatarajia kufanya Kongamano la Biashara, Uwekezaji na Utalii Mei 26, 2025, jijini Osaka, Japan ikiwa ni sehemu ya ushiriki wake katika Maonesho ya Dunia ya EXPO 2025 yatakayofanyika Osaka, Japani, kuanzia Aprili 12 hadi Oktoba 13, 2025.
Kongamano hilo linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la majadiliano na ushirikiano baina ya Tanzania na wawekezaji wa kimataifa, hususan kutoka Japan.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 16, 2025 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo amesema kongamano hilo litawaweka pamoja wadau kutoka sekta mbalimbali duniani, na kuwa ni jukwaa muhimu kwa Tanzania kuonesha fursa zilizopo kwa ajili ya kuvutia uwekezaji nchini na kuweka ushirikiano wa kimkakati.
Amesema Kongamano hili litafanyika siku moja baada ya “Siku ya Kitaifa ya Tanzania” itakayoadhimishwa tarehe 25 Mei 2025, ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
“Tanzania itakuwa na banda la maonyesho lenye ukubwa wa mita za mraba 53, pamoja na eneo la biashara la mita za mraba 15 kwa ajili ya kukuza bidhaa na huduma za ndani…. Zaidi ya washiriki 500 kutoka sekta mbalimbali wanatarajiwa kushiriki, huku 300 wakiwa tayari wameishajisajili.
Maonesho haya yanatarajiwa kuvutia zaidi ya wageni milioni 28.2 kutoka kote duniani, na hivyo kutoa jukwaa muhimu kwa Tanzania kuonyesha vivutio vyake vya kiutalii, miradi ya kimkakati ya miundombinu, na fursa za uwekezaji katika sekta kama Kilimo, afya utalii, Uchumi wa Bluu na nyinginezo.
“Katika banda la Tanzania Taasisi zinapaswa kuwasiisha maudhui yaliyo katika mfumo wa Makala na maandiko ya miradi ya kimkakati yenye kuvutia biashara, uwekezaji na utalii,” amesema Waziri Jafo .
Amesema, katika kongamano hilo, sekta mbalimbali zitapewa kipaumbele ikiwemo Miundombinu, Nishati, Kilimo, Uchumi wa Buluu, Utamaduni na Teknolojia. Lengo kuu ni kuonesha fursa zilizopo nchini Tanzania na kuvutia wawekezaji wapya pamoja na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na biashara kati ya Tanzania na mataifa mengine duniani.
Waziri Jaffo amesema kuwa kongamano hilo linaratibiwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia TANTRADE kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali na sekta binafsi. Serikali inatoa wito kwa taasisi, mashirika na wadau mbalimbali kushiriki kikamilifu katika maandalizi na ushiriki wa kongamano hilo kwa manufaa ya taifa.
“Ni muhimu sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kongamano hili, kwani wao ndio watakaoleta bidhaa na huduma halisi zitakazowavutia washiriki wa kimataifa”. Amesema waziri Jafo
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angelina Ngalula, amesema ushiriki wa Tanzania utatangaza fursa za kibiashara, uwekezaji, utalii na ubunifu katika mawanda ya ulimwengu.
“Sekta binafsi imejiandaa sio tu kushiriki, bali pia kuuza fursa za kiuchumi zinazoifanya Tanzania kuwa mahali bora kwa biashara na uwekezaji.” Amesema Angelina
Amesema Taasisi hiyo imejipanga kwa kuhakikisha wanakwenda kutangaza bidhaa za kilimo za Tanzania zikiwemo korosho, kahawa na chai, zinapata nafasi ya kuoneshwa katika maonesho hayo, kama njia ya kuimarisha mauzo ya nje na kukuza uchumi wa nchi.
“Tutaenda Osaka tukiwa tumebeba mazao bora ya kilimo kutoka Tanzania, tunataka dunia ijue kuwa Tanzania ni lango la bidhaa bora na fursa nyingi za kiuchumi,” amesema Angelina
Angelina ameeleza kuwa kutokana na uzoefu wa mafanikio katika Expo 2020 Dubai ambapo kampuni 500 za Tanzania ziliweza kushiriki na kufanikisha mikataba 36 yenye thamani ya dola bilioni 8 za Kimarekani, matarajio ya mwaka huu ni makubwa zaidi. Takribani kampuni 500 zinatarajiwa kushiriki Osaka EXPO, huku idadi ya watembeleaji ikitarajiwa kufikia milioni 28.2, wakiwemo milioni 3.5 kutoka nje ya Japan.
Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika Expo iliyopita ni ajira 214,575 zilizozalishwa kupitia sekta mbalimbali, upatikanaji wa masoko katika maduka makubwa ya kimataifa kama Lulu Hypermarket, pamoja na vijana wa Kitanzania kupata ubia na makampuni ya kimataifa.
“Tunataka Osaka Expo 2025 kuwa ya kihistoria kwa Tanzania. Kama Dubai tuliweza kuvutia uwekezaji wa zaidi ya dola bilioni 8, safari hii tunaamini tunaweza kuvuka bilioni 10.” Amesema Angelina
