Na WMJJWMM, Tarime – Mara
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Felister Mdemu amewaasa wananchi kutumia mikopo inayotolewa na Serikali ili kujikwamua kiuchumi kwa maendeleo ya familia zao na jamii inayowazunguka.
Felister ameyasema hayo Aprili 15, 2025 kwenye mkutano na wakazi wa Kata ya Susuni, Bumera, Mwema na Sirari za Wilaya ya Tarime Mkoani Mara. Mkutano huo ni muendelezo wa Kampeni ya Mageuzi ya Kifikra na Mtazamo wa kuwafanya wananchi kuwa kitovu cha maendeleo yao.
Amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ni sikivu, imetenga pesa kupitia mifuko mbalimbali ya uwezeshaji kiuchumi hivyo, amewasisitiza wananchi kuchangamkia fursa hizo ili kujikwamua kiuchumi.
” Nisisitize na wale wote ambao wamenufaika na mikopo kuhakikisha mikopo hiyo imekuwa chachu kwao ya kupiga hatua za maendeleo na si vinginevyo” amesema Felister.
Aidha, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia, kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Juliana Kibonde amesema Serikali imeanzisha mifuko mbalimbali iliyoanzishwa ya kuwawezesha wananchi kupata mikopo yenye riba nafuu ikiwemo mfuko wa vijana, mfuko wa vikundi vya wafanyabishara, mfuko wa kundi la wenye mahitaji maalum wakiwemo walemavu na mfuko wa wanawake.
“Mifuko yote hii imeletwa kwa ajili ya kuwasaidia kuboresha na kuanzisha miradi mbalimbali, hakikisheni mnakidhi vigezo ikiwa pamoja na kuanzia vikundi ili muweze kunufaika na mikopo hii yenye riba nafuu” amesema Juliana
Mmoja wa mnufaika wa mikopo hiyo Erick Odhiambo amesema ametumia fursa ya mkutano huo kutoa hamasa kwa wananchi ya namna alivyonufaika na Mikopo inayotolewa na Serikali kwa masharti nafuu ili kuwa utia wananchi wenzake kupata mikopo hiyo na kuondokana na mikopo isiyo na tija inayowakandamiza.
“Mimi ni shahidi na mnufaika wa hii mikopo inatusaidia sana, awamu ya kwanza nilifanikiwa kupata mkopo wa shilingi milioni tano (5 ), baada ya kukamilisha marejesho nikufuzu kuchukuwa awamu ya pili kiasi cha shilingi milion sita (6) fedha ambazo zimenisaidia kulima, kujenga nyumba na kupanua biashara yangu ya ushonaji.” ameeleza Odhiambo.