Waandishi wa habari wanawake nchini wametajwa kuwa miongoni mwa waathirika wakubwa wa ukatili unaotokana na unyanyapaa na ubaguzi wa kijinsia, hali inayochangia kuathiri ubora wa kazi zao pamoja na ustawi wao wa kisaikolojia.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mawasiliano na Habari wa Tume ya Taifa ya UNESCO Tanzania, Christina Musaroche, kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Profesa Hamisi Malebo Masanja, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari jijini Mwanza.
“Ukatili huu umebainika kuwa chanzo cha msongo wa mawazo, mfadhaiko, na woga wa kushiriki mijadala ya umma. Aidha, husababisha waandishi wanawake kukosa kujiamini na kupoteza ari ya kazi, jambo linaloathiri kwa kiasi kikubwa ubora wa kazi zao,” amesema.
Aidha, ameongeza kuwa hali hiyo inapaswa kushughulikiwa kwa nguvu zote kupitia ushirikiano wa taasisi mbalimbali, serikali, na wadau wa habari ili kuhakikisha usalama wa wanahabari wote, hasa wanawake.
Kwa upande wao, baadhi ya waandishi walioshiriki mafunzo hayo wameeleza changamoto wanazokutana nazo kazini, huku wakipongeza juhudi za UNESCO katika kuandaa mafunzo hayo na kutoa wito wa kuendelezwa kwa programu kama hizo katika mikoa mingine.
Mafunzo hayo ni mkakati wa kimataifa wa kulinda haki na usalama wa waandishi wa habari, hususan wanawake, ambao mara nyingi hukumbana na changamoto nyingi zisizoonekana hadharani

