Na Silivia Amandius,
Bukoba.
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mhe. Erasto Sima, amelaani vikali vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, hususan ubakaji na ulawiti dhidi ya watoto vinavyoendelea kuripotiwa wilayani humo.
Akizungumza Aprili 17, 2025 katika kikao cha baraza la madiwani la robo ya tatu kilichofanyika katika Ukumbi wa Chemba, Mhe. Sima alieleza kusikitishwa na ongezeko la matukio hayo, huku baadhi ya wazazi – hasa wanaume – wakitajwa kuwa sehemu ya tatizo.
“Sasa hivi ndoa zikivunjika, kina mama wanaondoka na kuwaacha watoto kwa baba zao. Cha kusikitisha ni kwamba baadhi ya baba hawa wamekuwa wakibaka watoto wao wa kuwazaa,” alisema kwa uchungu.
Alieleza kuwa tayari kuna tukio la kusikitisha la baba mmoja aliyetelekezwa na mke wake, na kubaki na binti yao wa darasa la sita, kisha kuanza kumtendea ukatili wa kingono na kumchukulia kama mke.
Mhe. Sima alifuatilia tukio hilo akiwa ameambatana na Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) pamoja na Afisa Usalama. Walipofika nyumbani kwa mtuhumiwa, walikuta barua ya msichana huyo aliyokuwa ameandika kwa Shangazi yake, akiomba achukuliwe akaishi naye kwa kuwa baba yake amekuwa akimfanyia vitendo vya unyanyasaji.
Kutokana na tukio hilo na mengine mengi yanayoripotiwa, Mhe. Sima alitoa wito kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama, viongozi wa dini, wazazi, na jamii kwa ujumla kushirikiana kwa karibu katika kutokomeza vitendo hivi ambavyo ni kinyume na sheria, maadili na utu wa mwanadamu.