Taharuki imeikumba jamii ya Kijiji cha Mipotopoto, kilichopo pembezoni mwa Pori la Akiba la Liparamba, wilayani Nyasa mkoani Ruvuma, kufuatia kuibuka kwa simba wa ajabu mwenye rangi isiyo ya kawaida ya mchanganyiko wa kahawia na nyeupe, ambaye alivamia makazi ya watu na kusababisha madhara mbalimbali kabla ya kuuawa na askari wa wanyamapori.
Kwa mujibu wa Diwani wa Kata ya Mipotopoto, Mheshimiwa Said Mahamud, tukio hilo lilianza siku nne zilizopita ambapo mkazi mmoja alinusurika kifo kwa miujiza baada ya kukutana ana kwa ana na mnyama huyo akiwa njiani kutoka shambani. Mkazi huyo aliweza kujiokoa kwa kupanda juu ya mti na kujificha hadi hatari ilipopita.
Simba huyo, ambaye anadaiwa kuwa na umbile kubwa na dalili za kudhoofika kiafya, aliendelea kuleta hofu katika kijiji hicho kwa matukio yaliyofuata, yakiwemo kuvamia nyumba na kuiba mbwa pamoja na baadhi ya nguo, na hatimaye kushambulia zizi la mifugo ambapo aliuwa kondoo watano na mbuzi mmoja.
Baada ya matukio hayo, serikali ilituma askari wa wanyamapori kutoka kituo cha Mbinga kwa ajili ya kuchukua hatua. Askari hao waliweza kumfuatilia simba huyo hadi walipomdunga risasi na kumuua, huku ngozi yake ikichukuliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kisayansi.
Diwani Mahamud amesema tukio hilo ni la kipekee na halijawahi kushuhudiwa katika eneo hilo kwa miongo kadhaa, tangu hifadhi ya Liparamba ilipoanzishwa. Ameeleza kuwa pamoja na huzuni ya kupotea kwa kiumbe adimu duniani, wananchi wamepata faraja kwa kurejeshwa kwa hali ya usalama kijijini.
Wataalamu wa wanyamapori wanasema simba wenye rangi hiyo ni nadra sana na huonekana katika maeneo maalum tu duniani, na Pori la Akiba la Liparamba likitajwa kuwa mojawapo ya maeneo hayo machache.
Tukio hili limezua mjadala mpana kuhusu uhusiano kati ya wanyamapori na jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi, huku wengi wakitaka kuwepo kwa mikakati madhubuti ya usalama na uhifadhi endelevu wa viumbe hai.