Na Belinda Joseph, Ruvuma.
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) imetoa pongezi kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma kufuatia kukamatwa kwa watuhumiwa wawili waliodaiwa kuhusika na wizi wa mita za maji na vifaa vingine vya miundombinu ya maji, mali ya mamlaka hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa SOUWASA, Mhandisi Patrick Kibasa amesema taasisi hiyo imekuwa ikikumbwa na changamoto kubwa ya wizi wa mita za maji kwa muda mrefu, hali iliyokuwa ikisababisha usumbufu mkubwa kwa wateja.
“Kwa siku tumekuwa tukiibiwa mita zisizopungua saba, na hadi sasa zaidi ya mita 185 zimepotea, jambo lililotupelekea kutumia zaidi ya shilingi milioni 50 kuziba mapengo ya hasara hiyo na kuhakikisha huduma zinaendelea kwa wananchi,” alisema Kibasa.
Mhandisi Kibasa, amesema mafanikio ya operesheni hiyo ni ishara ya dhamira ya kweli ya Jeshi la Polisi katika kulinda miundombinu ya taifa huku akitoa wito kwa wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama pamoja na SOUWASA katika kuhakikisha miundombinu hiyo inalindwa, amesisitiza kuwa mafanikio haya ni hatua muhimu kwa mamlaka hiyo na jamii kwa ujumla, akilisisitizia Jeshi la Polisi kuendelea na operesheni kama hizo ili kutokomeza kabisa vitendo vya uharibifu wa miundombinu.
Akizungumza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma SACP Marco Chilya, amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Idrisa Mnimi (21) na Ramadhani Athuman Kalumbu (19), wote wakazi wa Songea ambapo Watuhumiwa hao walikamatwa tarehe 11 Aprili 2025 katika Mtaa wa Matarawe, Manispaa ya Songea, wakiwa na vifaa mbalimbali vya maji vilivyoibwa kutoka maeneo tofauti.
Amevitaja Vifaa vilivyokamatwa ni pamoja na mita za maji 27, cover meter 8, ball corki 161 na ball valve 77 – vyote vikiwa mali ya SOUWASA, amesema upelelezi bado unaendelea na juhudi za kuwasaka wahalifu wengine waliohusika katika mtandao huo wa wizi zinaendelea.
Kiujumla, kupatikana kwa watuhumiwa hao kumetajwa kuwa ni hatua kubwa katika juhudi za SOUWASA na Jeshi la Polisi Mkoani Ruvuma kuwa na ushirikiano na juhudi kubwa katika kuwabaini wahusika wa vitendo hivyo, kuwachukulia hatua za kisheria na kuhakikisha miundombinu ya maji inaendelea kutunzwa.