
Na Nihifadhi Abdulla Zanzibar
LICHA ya Zanzibar kuwa na idadi kubwa ya wanawake kwa asilimia 52 ya wakazi wake, wanawake bado ni wachache mno katika nafasi za maamuzi. Hali hii inasababisha maswali kuhusu utekelezaji halisi wa usawa wa kijinsia unaozungumzwa kila mara.
Katika kuhakikisha Wanawake wanapata haki ya uongozi kwakuzingatia usawa wa kijinsia wanaharakati mbalimbali wanaendelea kupaza sauti kueleza kwa nini nafasi hizi bado ni finyu kwa wanawake, licha ya uwepo wa katiba, mikataba ya kimataifa na sera zinazolenga kutoa haki sawa.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 21, pamoja na Katiba ya Zanzibar, zinatamka wazi kuwa kila raia ana haki sawa ya kushiriki kwenye uongozi wa nchi. Lakini hali ya vitendo bado ni tofauti kabisa.
Mikataba ya kimataifa kama CEDAW na ule wa SADC unasisitiza usawa wa kijinsia asilimia 50/50 katika vyombo vya maamuzi, lakini utekelezaji wake bado unalegalega ndani ya mfumo wa kisiasa wa Zanzibar.
Mwanaharakati wa haki za wanawake na mtetezi wa demokrasia, Almas Muhamed, anaeleza kuwa “ushiriki wa wanawake katika nafasi za maamuzi ni jambo la msingi kwa maendeleo ya kweli ya jamii. Bila sauti ya mwanamke mezani, maamuzi hayatawakilisha wote.”
Pamoja na hayo anasisitiza kuwa bila mikakati madhubuti ya kuanzia ngazi ya chini, hakuna mabadiliko ya kweli yatakayopatikana. “Lazima tuanze na mabadiliko ya mtazamo wa jamii kuhusu uwezo wa mwanamke katika kuongoza huku tukinasibisha namifano hai ya uongozi wao hapo tutapata njia”anamalizia Almas.
Takwimu za mwaka 2020 zinaonesha kuwa madiwani wanawake walikuwa asilimia 23 tu, huku Baraza la Wawakilishi likiwa na wanawake wanane tu kati ya 50 walioteuliwa kupitia uchaguzi wa moja kwa moja.
Vilevile, kati ya majimbo yote ya uchaguzi Zanzibar, wanawake walioweza kushinda kwa kura za wananchi ni wachache mno, jambo linaloonyesha changamoto kubwa wanazokumbana nazo wakati wa kampeni na uchaguzi.
Wanasiasa wanawake waliowahi kugombea nafasi mbalimbali wameeleza changamoto wanazokumbana nazo, ikiwa ni pamoja na upinzani wa kijamii, ukosefu wa rasilimali, na kutopata sapoti kutoka ndani ya vyama vyao.
Asha khalfan akiwa ni mmoja wao anaeleza laity vyama vingewaunga mkonoidadi ya wanawake viongozi ingepanda “Tulitegemea vyama vyetu vitasimama nasi, lakini hatukupata mafunzo wala maandalizi ya kisiasa ya kutosha. Tuliingia kwenye uwanja wa vita bila silaha hii ikawa njia ya kutofika mbele.”
Mjumbe wa kamati ya siasa ya chama cha mapinduzi CCM Salum Mwinyi ameeleza kikwazo kikubwa kwa wanawake kuwa kidogo kwenye uongozi inatokana na kutokuwa na uzoefu ndani ya chama “niwanahimize kuanza kujihusisha na siasa kuanzia ngazi za shina, tawi, wilaya hadi taifa, kwani kwa kufanya hivyo watajenga uzoefu na uhalali wa kugombea nafasi kubwa zaidi siku zijazo”anamalizia Mwinyi.
Kwa upande mwingine, mwanamke aliyeshinda kwenye uchaguzi na kuingia madarakani Zawadi Amour Mwakilishi wa jimbo la Konde Pemba ameeleza changamoto alizokutana nazo, “mimi nilitengwa karibia na kila mtu wengi wao ni baadhi ya viongozi wa kiume na huzushiwa mambo ambayo sijawahi hata kufanya
Lakini alibainisha kuwa hakukata tama “sikuvunjika moyo na familia iliendelea kuniunga mkono na kusimama na mimi kidete na ndio maana nikafanikiwa”anamalizia Zawadi.
Afisa mipango na jinsia wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC Lutfia Faida Haji ameeleza kuwa tume inachukua hatua kupitia kampeni za elimu ya mpiga kura zenye mlengo wa kijinsia, huku ikiweka mazingira rafiki ya wanawake kuchukua fomu na kushiriki uchaguzi kwa usawa.
“Tunalenga kuondoa vikwazo vinavyowakwamisha wanawake kujiandikisha au kugombea, lakini jamii nayo inatakiwa kubadilika kuelekea uchaguzi huu 2025wanawake wanapaswa kuendelea kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi .”anasema Lutfia
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA ZNZ Dkt Mzuri Issa anasema wamekuwa mstari wa mbele kuelimisha jamii na kuwajengea uwezo wanawake kugombea nafasi za uongozi.kwa kushirikiana jumuiya ya wanawasheria wanawake Zanzibar ZAFELA na PEGAO “kwa pamoja tunatoa mafunzo, tunawasimamia katika maandalizi ya kugombea kuwa na ujasiri wa tunapaza sauti zao katika majukwaa ya maamuzi.”
Mwisho wa yote, vyama vya siasa, jamii, na taasisi za serikali zinapaswa kushirikiana kwa dhati kuweka mazingira rafiki kwa mwanamke, si tu kwa kumsaidia kushinda uchaguzi, bali pia kuhakikisha anathaminiwa kwenye nafasi hiyo ya uongozi.