*Asisitiza Chama hakiwezi kukubali mtu au kikundi cha watu kuvuruga amani iliyopo
Na Mwandishi Wetu, Tabora
MAKAMU Menyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Stephen Wasira, amesema ni vema wananchi wakafahamu kwamba katika amani ndani yake kuna haki, hivyo Chama kitaendelea kuihubiri kuhakikisha inapatikana haki.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mjini Dodoma alipokuwa akihitimisha ziara yake katika Mkoa wa Tabora, jana, Wasira amesema kuna watu wanahoji CCM inazungumzia sana amani lakini haizungumzii haki, huku akibainisha kuwa wanaotoa madai hayo ni watu wazito.
“Sasa nikasema ngoja niende (Tabora) kwenye kitovu ambapo Mwalimu Julius Nyerere alitoa machozi kwa ajili ya amani, tuwasaidie kuelewa kwamba ukizungumza amani ndani ya amani kuna haki kwa sababu amani ikikosekana wenye uwezo mdogo wanaumia.
“Amani ikikosekana wanawake na watoto wao katika nchi jirani wanakilimbilia Tabora…ukilinda amani unalinda haki tena unalinda haki ya wanyonge, unalinda haki ya wasiokuwa na sauti.
“Unazungumza haki ya mtu anasema anataka kuwa Rais halafu anaambiwa eti tukibadili Katiba anakuwa Rais na haki inayosemwa ni mtu mmoja badala ya kuzungumza haki ya walio wengi. Tunauliza huyo anayesema hatuzungumzi haki tunazungumza amani sijui anadhani ndani ya amani hakuna haki.” Amesema Wasira.
Ameongeza kuwa kote ambako amani imekosekana haki ya wengi imepotea hususan nchi za jirani wananchi wake walikimbilia Tanzania, hivyo alihoji iwapo ikitokea amani iliyopo kukumbwa na dhoruba Watanzania watakimbilia wapi
“Wenyewe wamekimbia kwao na ninyi mnataka kukimbilia kwao mnapishana kama sisimizi. Hivyo tunasisitiza haki lakini haki iko ndani ya amani. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka vyombo na inasema kazi ya Bunge ni kutunga sheria, kazi ya Mahakama ni kutafsiri sheria na kuweka haki na haki hiyo ni haki ya kibinadamu, hatuzungumzi haki ya Mungu.
“Tumeweka mahakama kwamba ndio inayolinda haki za watu, sasa kama wewe unadhani hupewi haki uende kwenye mahakama ukadai hiyo haki yako usikilizwe ili ulete amani na upate haki yako kwa njia ya amani
“Unatuambia utakinukisha, unatuambia utaichoma Tanzania nani anakupa leseni ya kuichoma Tanzania? Kwa idhini ya nani? Ndio maana tunawaambia wale wanaotaka kutumia nguvu tutawaambia hiyo sio njia halali unataka kuvunja haki ya wanyonge wa Watanzania
“Unataka kutengeneza matatizo yatakayofanya akinamama wakimbie kliniki na kliniki tulizowajengea zibomolewe kwa mabomu, hivyo hatuwezi kukubali hilo. Nawashangaa Watanzania ambao hawajaelewa na wakiwasikiliza wanawapigia makofi lakini hawajui gharama zake,” amesema Wasira.
Hivyo amewaambia wananchi kuwa ameamua kuwachochea Watanzania kupitia Tabora ambako ni chimbuko la amani iliyowekwa nchini kwa machozi ya Julius Nyerere kwamba amani hiyo lazima itadumu kwa gharama yoyote.
“Hatuwezi kuruhusu watu wachache au kikundi kinachotumwa na vibaraka na Wakoloni mambo leo kuja kuvuruga amani ya nchi yetu, hatutafanya hivyo. Narudia kuna amani na ndani ya amani kuna haki.