Na Silivia Amandius
Kyerwa, Kagera.
Afisa dawati wa Msaada wa Kisheria kutoka Kampeni ya Mama Samia, Rajabu Dauda Mussa, amewataka wajumbe wa mabaraza ya ardhi kuhakikisha wanatunza siri za wananchi wanapotekeleza majukumu yao ya kisheria katika jamii.
Akizungumza katika mkutano wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Kyerwa uliofanyika katika ukumbi wa CCM wilayani humo, Mussa aliwataka pia wenyeviti wa vijiji na vitongoji kuwa mstari wa mbele katika kusuluhisha migogoro ya ardhi na mingine inayowakabili wananchi wao.
“Ni muhimu viongozi wa vijiji na vitongoji kuwa na mikutano ya mara kwa mara na wananchi wao, angalau kila baada ya miezi mitatu, ili kutoa elimu na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi,” alisema Mussa.
Aidha, aliihimiza Jumuiya ya Wazazi ya CCM Kyerwa kuhamasisha wananchi kuchangamkia fursa ya msaada wa kisheria kupitia kampeni ya Mama Samia, akieleza kuwa kampeni hiyo inalenga kuimarisha maendeleo ya wananchi na halmashauri kwa ujumla.
“Hii ni fursa ya wazazi pia, hivyo ninyi kama jumuiya mna wajibu wa kuhamasisha kata zenu kushiriki kikamilifu kwani kampeni hii inalenga kuondoa vikwazo vya upatikanaji wa haki hasa kwa wanyonge,” aliongeza.
Kwa upande wake, Ndugu Mzakiru Hamza ambaye ni Paralegal na msaidizi wa kisheria katika kampeni hiyo, aliwahimiza wananchi kujenga utamaduni wa kutatua migogoro kwa busara badala ya kuchochea migongano zaidi.
“Migogoro mingi inaweza kuepukika iwapo tutatumia hekima na mazungumzo. Kampeni hii inalenga kuwapa wananchi maarifa ya kisheria ili wajue namna bora ya kutafuta suluhu,” alisema Hamza.
Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia ni mpango wa kitaifa unaolenga kuwafikia wananchi wa ngazi ya chini hasa vijijini, kwa kuwapa msaada wa kisheria bila gharama ili kuongeza upatikanaji wa haki kwa usawa.