Wakazi wa Kata ya Gongolamboto jijini Dar es Salaam wametoa shukrani zao kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa kutoa msaada wa shilingi 8,915,000 kwa ajili ya ujenzi wa kivuko kilichokuwa kinasababisha usumbufu mkubwa kwa wakazi wa eneo hilo hasa wakati wa mvua kubwa.
Hatua hiyo imekuja kufuatia ombi lililotolewa na uongozi wa Kata ya Gongolamboto kwa TRC, kufuatia changamoto iliyojitokeza baada ya ujenzi wa tuta la reli ya kisasa (SGR) uliosababisha kuzibwa kwa njia ya asili ya maji kutoka eneo la Uwanja wa Chuo cha Kampala kuelekea kwenye reli hiyo.
Akizungumzia tukio hilo, Afisa Mtendaji wa Kata ya Gongolamboto, Bw. Majura Mtelemwa, amesema kuwa msaada huo umetolewa kwa wakati muafaka, na utaondoa usumbufu uliokuwa ukiwakumba wakazi wa mtaa wa Gongolamboto, ambao walikuwa wanakabiliwa na mafuriko na ugumu wa kupita kutokana na maji kutuwama.
“Baada ya ujenzi wa tuta, maji yalikuwa yanajaa na kufanya watu washindwe kupita, Ilikuwa ni kero kubwa kwa wananchi. Tunashukuru TRC kwa kuonesha ushirikiano na kutusaidia kutatua tatizo hili,” amesema Mtelemwa.
Ameongeza kuwa TRC wameonesha uwajibikaji na nia ya dhati ya kusaidia jamii kwa kukubali ombi lao na kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa njia ya maji asilia, hatua ambayo imesaidia kuleta matumaini na utulivu kwa wakazi wa eneo hilo.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, Mhandisi Tadeo Paul, amesema kuwa mkandarasi tayari amewasili katika eneo la kazi na hatua za awali za maandalizi ya ujenzi wa kivuko zimeanza.
“Tunatambua umuhimu wa eneo hili kwa jamii. Tupo pamoja nao na tayari tumeanza taratibu za ujenzi ili kuhakikisha changamoto hii inatatuliwa haraka,” amesema Mhandisi Tadeo.
Wananchi wa Gongolamboto sasa wana matumaini makubwa kuwa ujenzi wa kivuko hicho utarejesha hali ya kawaida na kurahisisha shughuli zao za kila siku, huku wakipongeza TRC kwa kujali maslahi ya jamii inayoishi karibu na mradi wa reli ya kisasa.