Na WAF – Songea, Ruvuma
Wananchi zaidi ya 900 wamepatiwa huduma za uchunguzi na matibabu ya ugonjwa wa saratani bila malipo katika Hospitali ya MT. Joseph Peramiho, huduma ambazo kutolewa na madaktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa muda wa siku nne (4).
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Aprili 19, 2025 alipotembelea kambi maalum ya uchunguzi wa magonjwa ya saratani ikiwemo saratani ya matiti na tezi dume katika Hospitali ya Mtakatifu Joseph Peramiho Mkoani Ruvuma inayoendelea hadi tarehe 20 Aprili, 2025 ikiwa leo ni siku ya tano (5).
“Watu 18 wamegundulika kuwa na viashiria vya ugonjwa huo ambapo 12 ni wanawake ambao tayari wameshapatiwa matibabu na sita (6) ni wanaume ambao wamepewa rufaa ya kwenda kufanyiwa uchunguzi zaidi, tuna kila sababu ya kumshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya haya yote kwa sababu ya kujali uhai wa maisha ya Watanzania,” amesema Waziri Mhagama.
Aidha, Waziri Mhagama amesema taarifa ya utafiti ya Tume ya Saratani (Oncology Commission Report) iliyozinduliwa nchini tarehe 26 Septemba, 2022 ilionesha kwamba nchi zilizopo kusini mwa jangwa la Sahara ziko hatarini kupata idadi kubwa ya vifo kutoka 520,348 hadi 1,000,000 kufikia mwaka 2030 endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa.
“Takwimu za Taifa kwa miaka mitano (5) kuanzia mwaka 2019 – 2024 zinaonesha kuwa aina za saratani zinazoongoza ni saratani ya mlango ya kizazi kwa asilimia 41, saratani ya matiti kwa asilimia19, saratani ya utumbo mkubwa na mdogo kwa asilimia 6.1, saratani ya koo kwa asilimia5.7 pamoja na saratani ya kichwa na shingo kwa asilimia 4.3,” amesema Waziri Mhagama.
Katika kuendelea kujikinga na magonjwa hayo, Waziri Mhagama amewataka wananchi kuchukua hatua kwa kuzingatia ulaji unaofaa ikiwemo kupunguza ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, chumvi nyingi na sukari, kuacha tabia bwete, kuacha vilevi pamoja na kuwa na tabia za kupima afya zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt. Diwani Msemo amesema lengo la kambi hiyo maalum ni kutoa elimu inayosababisha saratani, uchunguzi wa saratani za awali pamoja na matibabu yake kwa wananchi.
“Kutokana na ushirikiano tulioupata katika hospitali hii, tumeamua kuwachukua wataalam kama wanne (4) hapa twende nao Ocean Road tukawafundishe namna ya kutoa huduma za saratani ili waje waendelee kutoa huduma hizo hapa kwakuwa pia kuna wagonjwa wanaokuja hapa kutoka nchi jirani.
Naye, shuhuda wa ugonjwa wa Saratani Bw. Cedou Mandingo (Babuu wa kitaa) amewashauri wananchi kuchukua hatua za haraka kwa kuchunguza afya zao mara kwa mara iwapo ikigundulika wana viashiria vya ugonjwa huo ili kuwahi mapema kupata matibabu kwakuwa ugonjwa huo unatibika na unapona.
“Ni jukumu letu sisi mabalozi tuwe na utaratibu wa kwenda katika vituo vya afya kutoa elimu ili wananchi wengi wajitokeze kufanya uchunguzi wa Saratani, mimi sijapona saratani kwa waganga wa nje ya nchi, nimepona hapa hapa nchini sababu ya uwepo wa watalam wa afya wabobezi waliowezeshwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hasaan, amini kwamba saratani inatibika na unapona ukiwahi mapema,” amesema Bw. Mandingo.