Na Silivia Amandius, Kagera
Viongozi wa dini wamemshukuru na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha na kushusha huduma ya msaada wa kisheria hadi ngazi ya vijiji na vitongoji, wakisema ni hatua muhimu kwa wananchi wengi wasio na uwezo wa kupata huduma hiyo.
Wakizungumza katika ibada ya Pasaka iliyofanyika katika moja ya nyumba za ibada iliyopo Kata ya Omurushaka, Mchungaji Bi. Odetha aliwahimiza waumini kutumia vizuri fursa hiyo kwa kutoa ushirikiano unaohitajika, kwani msaada wa kisheria ni haki ya kila mwananchi.
Aidha, alitoa wito maalum kwa wanawake waliokumbwa na changamoto katika ndoa na familia, hasa upande wa matunzo ya watoto, kutumia huduma hiyo kutafuta haki zao kwa njia ya amani na kisheria.
Baadhi ya waumini walioshiriki ibada hiyo, akiwemo Ndugu Bobmare France Kabilinda, waliipongeza kampeni hiyo kwa kuwawezesha kueleza maoni na changamoto zao. Miongoni mwa changamoto walizozitaja ni pamoja na ukosefu wa vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa zaidi ya miaka mitatu na baadhi ya viongozi wa vijiji kujimilikisha madaraka yasiyo yao.
Wananchi wametakiwa kuendelea kushiriki kwa wingi katika huduma hiyo ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wote.