KAMPUNI Airtel Tanzania imejivunia kutangaza kuendeleza udhamini wake kwa Klabu ya Singida Black Stars, ambapo safari hii udhamini huu unalenga kuisaidia timu hiyo katika mashindano ya Kombe la Muungano 2025, yatakayofanyika visiwani Zanzibar. Hatua hii inaonyesha dhamira thabiti ya Airtel katika kukuza michezo na kuendeleza soka nchini Tanzania.
Kama ilivyokumbukwa, Airtel Tanzania ilisaidia ujenzi wa uwanja wa kisasa wa timu hiyo, maarufu kama Airtel Stadium, kupitia udhamini wake wa awali. Safari hii, Airtel imetoa msaada wa kipekee kwa timu ya Singida Black Stars kwa kutoa jezi maalum kwa ushirikiano na Wakazi Limited, kampuni rasmi inayohusika na utengenezaji na usambazaji wa jezi za timu hiyo. Jezi hizi mpya zitatumika katika mashindano ya Kombe la Muungano 2025, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya timu hiyo kushindana kwa kiwango cha juu.
Akizungumzia udhamini huu, Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Jackson Mmbando, alisema: “Tunajivunia kuendelea kushirikiana na Singida Black Stars SC. Mchango wetu katika timu hii kuelekea Kombe la Muungano 2025 Zanzibar ni dalili ya imani yetu katika kukuza vipaji, kuleta mshikamano, na kuunganisha jamii kupitia michezo.”
Kwa upande wa Singida Black Stars, uongozi wa klabu umeonyesha shukrani zao kwa msaada endelevu kutoka Airtel, wakisema kwamba udhamini huu umeongeza ari ya timu na kuwapa motisha ya kuweka malengo makubwa katika mashindano ya kitaifa na kikanda.
Kombe la Muungano ni mashindano makubwa yanayokutanisha vilabu bora kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, yakilenga kukuza mshikamano wa kitaifa na ushindani wa kweli. Ushiriki wa Airtel katika mashindano haya unaendelea kudhihirisha nafasi yake kama mdau muhimu katika maendeleo ya michezo na ustawi wa jamii nchini Tanzania.