KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Mwenda amesema TRA itawachukulia hatua Kali kwa mujibu wa sheria waagizaji na wauzaji wa mafuta ya Petroli na Dizeli wanaokiuka taratibu za nchi kwa lengo la Kukwepa Kodi.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam leo Aprili 22 2025 katika kikao cha pamoja na wafanyabiashara wa makampuni mbali mbali ya usambazaji na uagizaji wa mafuta nchini Kamishna Mwenda amesema hawatawafumbia macho wanaojaribu kuharibu biashara hiyo kwa kukwepa Kodi.
Amesema wamekutana na Wafanyabiashara hao kwa lengo la kujadili namna bora ya wao kulipa kodi ili kuendelea kuchangia kuendesha shughuli za uchumi wa Taifa letu.
Kamishna Mwenda amesema wafanyabiashara hao wanamchango mkubwa katika kuendesha uchumi wa nchi na wanasaidia shughuli mbali mbali za kiuchumi zinazofanyika huku akibainisha kuwepo kwa taarifa za Wafanyabiashara wanaokwepa Kodi kwa kuuza nchini kinyemela mafuta yanayopaswa kwenda nchi nyingine yakipitia Tanzania.
“Kuna wachache ambao wanaleta mafuta kwa ajili ya nje ya nchi( Non BPS ) yanasemekana baadhi yao hayaendi yanapotakiwa yanaharibu soko na kuondoa ushindani, hao hatuwezi kuwaacha” Amesema Mwenda
Amesema mafuta yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi yanapaswa kukaa nchini ndani ya siku 30 na si vinginevyo.
“Tunataka kampuni zote zifuate taratibu zetu, nje ya hapo tutasimamia sheria bila kujali kwamba sijui wamepata vibali vya nani sisi tutasimamia sheria yetu ya Afrika Mashariki,”amesema Mwenda
Kuhusu mchango wa Kodi kwa Kampuni za mafuta Mwenda amesema zinachangia zaidi ya shilingi bilioni 400 kwa kila mwezi ambazo zinasaidia kuendesha uchumi wa nchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waagizaji na Wasambazaji wa Mafuta (TAOMAC), Raphel Mgaya amesema kuwa wanachokiona kwenye soko la mafuta kwa sasa hivi ni kutokuwepo kwa usawa kutokana na baadhi ya makampuni kuuza mafuta kwa Bei ya chini tofauti na Bei elekezi kwa sh. 400.
Amesema jambo hilo linadhoofisha ushindani na kuiomba TRA kuwasaidia kujua sababu za tofauti hiyo ya Bei iwapo wote wanafanya biashara halali.
Ameomba meli ya Mafuta ikifika bandarini waagizaji walipe asilimia 50 ya gharama na gharama nyingine zilipwe baada ya mzigo kuuzwa ili kusaidia kuimarisha tasnia ya Mafuta ambayo haijakaa sawa tangu kipindi cha Korona na kueleza kuwa wanayo Imani na TRA kwamba itawasaidia.