NJOMBE
Mkuu wa wilaya ya Njombe Juma Sweda ameonya walimu wanaochukua mikopo ya kausha damu na kuweka dhamana vyeti vyao vya taaluma na kujikuta wakitumbukia kwenye matatizo makubwa pindi wanaposhindwa kurejesha mikopo hiyo kwa wakati,hatua ambayo imekua na athari kubwa kitaaluma mashuleni kwani walimu wengi hulazimika kutofika vituo vyao vya kazi na kuishi mafichoni ili kuwakwepa wakopeshaji jambo ambalo limekuwa na athari kubwa kitaaluma.
Juma Sweda Ametoa wito huo wakati wa kufunga mkutano mkuu wa uchaguzi wa chama cha walimu(CWT)mkoa wa Njombe kwa niaba ya mkuu wa mkoa,ambapo anasema kuna haja ya kuanza kupeana fursa na elimu za ujasiriamali ili kukabiliana na wimbi la walimu kutumbukia kwenye mikopo umiza ambayo inawafanya kutohudhuria vipindi kwa lengo la kuwakwepa wakopeshaji jambo ambalo linatiliwa mkazo pia na wagombea wa nafasi mbalimbali
Wakati serikali ikionya walimu na mikopo hiyo umiza, Vingozi wapya waliopata dhamana ya kuongoza chama hicho hadi 2030 akiwemo Shaban Ambindwile ambae amechaguliwa tena kuwa mwenyekiti wa CWT Njombe na Thobias Sanga mjumbe wa kamati tendaji taifa wameahidi kwenda kupigania haki za walimu sambamba na kuwaunganisha na fursa za uchumi.
Kwa upande wao walimu walioshiriki uchaguzi huo akiwemo Mwl Philipo Ndimbo wamewapongeza viongozi wapya na kisha kuwakadidhi jukumu la kwenda kufikisha na kupigania changamoto zao.
Nae mwenyekiti wa CWT kitengo cha walimu wanawake mkoa wa Njombe Mwl Atuswege Mwambela amewashukuru wapiga kura kwa kumuamini kuongoza kitengo hicho kwa miaka mitano huku akisema atakuwa kiungo cha walimu wote,atakabiliana na mifumo dume ili kumuinua mwanamke,kufanya uongozi shirikishi na kuwaunganisha na fursa za uchumi walimu wanawake.