Amidi na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mheshimiwa Augustine Mwarija akizungumza na waandishi wa habari kando ya warsha hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam Aprili 23, 2025.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa, akifafanua mambo kadhaa ambayo taasisi ya BRELA imeyaeleza na kuwapa elimu ya Miliki Bunifu.
Mkurugenzi wa Utafiti, Muunganiko na Utetezi kutoka Tume ya Ushindani (FCC), Zaitun Kikula, akifafanua mambo kadhaa ambayo kama FCC wameyaeleza katika warsha hiyo ya majaji.
…………..
Majaji wa Mahakama ya Rufaa wamekutana jijini Dar es Salaam katika warsha maalum yenye lengo la kuwapa elimu kuhusu sheria zinazohusiana na miliki bunifu.
Akifungua warsha hiyo kwa niaba ya Jaji Mkuu, Amidi na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mheshimiwa Augustine Mwarija alisema kuwa warsha hiyo inalenga kuwajengea uelewa majaji wa Mahakama ya Rufaa kuhusu sheria za miliki bunifu, hasa ikizingatiwa maendeleo makubwa ya teknolojia katika karne hii.
“Malengo mengine ni pamoja na kuangalia matumizi ya teknolojia ya kisasa, historia ya miliki bunifu, na namna bora ya kulinda haki za watu wanaomiliki hati miliki,” alisema Jaji Mwarija.
Aidha, aliongeza kuwa kupitia warsha hiyo, majaji watapata fursa ya kujadili sheria zilizopo huku wakipata mada kutoka kwa wataalamu wa ndani na nje ya nchi, wakiwemo kutoka Kenya na Tanzania.
Amesema kuwa Mahakama ya Rufaa hupokea na kusikiliza mashauri yanayohusu migogoro ya miliki bunifu, ingawa kwa sasa idadi ya mashauri hayo bado ni ndogo kutokana na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu masuala hayo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa, alisema kuwa lengo la warsha hiyo ni kubadilishana mawazo na kuwajengea majaji uelewa wa kazi zinazofanywa na BRELA katika eneo la miliki bunifu.
“Kumekuwa na kesi nyingi zinazowasilishwa mahakamani kuhusu miliki bunifu, lakini changamoto imekuwa kwamba majaji wengi hawajawahi kukutana na masuala haya, jambo linalokwamisha upatikanaji wa maamuzi sahihi kwa wakati,” alisema Bw. Nyaisa.
Aliongeza kuwa elimu hiyo ni endelevu, na kwamba BRELA inashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Shirika la Miliki Bunifu Tanzania na shirika la Alipo katika kuwajengea uwezo majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa ili kuwawezesha kutoa maamuzi sahihi katika mashauri yanayohusu ubunifu.
“Tunaposema BRELA inalinda bunifu za Watanzania, tunamaanisha kuwa kesi zikifika Mahakama Kuu na mlalamikaji asiporidhika, hurejea Mahakama ya Rufaa. Ni muhimu kwa majaji wa Rufaa kuwa na uelewa wa kina kuhusu miliki bunifu,” alisisitiza.
Alihitimisha kwa kusema kuwa vyombo vya kimahakama vinapaswa kushirikiana na taasisi kama BRELA katika kulinda bunifu za Watanzania, kwani ubunifu ulioandikishwa hapa nchini unapata ulinzi wa kimataifa
Mkurugenzi wa Utafiti, Muunganiko na Utetezi kutoka Tume ya Ushindani (FCC), Zaitun Kikula, amesema kuwa kwa kushirikiana na WIPO na BRELA, warsha hiyo kwa Majaji wa Rufani ni muhimu katika mchakato mzima wa kulinda Miliki bunifu kulingana na mazingira ya biashara ya nchi.”
Mhe. Dkt. Paul. F. Kihwelo. Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto akizungumza katika warsha hiyo ya mauaji wa mahakama ya rufaa.