MAHAKAMA ya Tanzania imeendelea kuonesha dhamira yake ya dhati katika kuimarisha mifumo ya kisheria inayolenga kuboresha mustakabali wa ulinzi wa miliki bunifu (Intellectual Property), ili kuiwezesha nchi kushiriki kikamilifu na kwa ushindani katika uchumi wa dunia, hasa katika zama hizi za maendeleo ya kiteknolojia.
Dhamira hiyo imesisitizwa na Jaji Augustine Mwarija wa Mahakama ya Rufani kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania wakati akifungua warsha ya siku moja kwa ajili ya majaji wa mahakama ya rufani iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo Aprili 23, 20225.
Amesema madhumini ya warsha hiyo ni kutoa elimu kwa majai wa mahakama ya rufani kuhusiana na sheria zinazohusiana na miliki bunifu hasa katika karne hii ambapo kuna maendelea makubwa sana Katika teknolojia, Kuangalia matumizi ya teknolojia ya sasa sheria zilizopo na nama ya umiliki wa hati bunifi au kutunza haki za haki miliki.
Warsha hiyo imeandaliwa na Shirika la Kimataifa la Mali Miliki (WIPO), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa kushirikiana na Tume ya Ushindani (FCC).
Amesema kuwa warsha hiyo imelenga kutoa jukwaa la kutafakari kwa kina juu ya mabadiliko na changamoto za sasa zinazohusiana na masuala ya miliki bunifu kwa kutambua kuwa eneo hilo si la kisheria tu bali ni nguzo muhimu katika maendeleo, biashara na ushirikiano wa kimataifa.
Ameeleza kuwa maendeleo makubwa ya kiteknolojia yamekuwa yakikimbia kasi ya mfumo wa sasa wa sheria za haki miliki, na hivyo warsha hiyo imelenga kupitia namna mfumo huo unavyoweza kufanyiwa marekebisho ili kuendana na mazingira ya sasa na kukabili changamoto kwa maarifa sahihi.
“Maendeleo haya ya kasi ya kiteknolojia, hasa katika nyanja ya Akili Bandia (AI), yanatoa changamoto kubwa kwa misingi ya kisheria iliyopo,” amesema Jaji Mwarija na kuongeza kuwa, “Mabadiliko haya ya kimapinduzi yanatulazimu kutathmini upya misingi ya kisheria ya jadi, kuhakikisha kuwa inabaki kuwa na umuhimu na uwezo wa kushughulikia changamoto katika dunia ya kidijitali inayobadilika kwa kasi.”
Amesema makutano kati ya Miliki bunifu na Akili Bandia yanabadilisha sekta mbalimbali, kuchochea uhitaji wa mahakama kutafakari upya tafsiri za kisheria ili kuendelea kuwa husika katika mazingira ya kisasa yanayoongozwa na ubunifu. “Wajibu wetu mkubwa ni kuhakikisha kuwa mifumo yetu ya sheria inaendana na wakati, inastahimili mabadiliko, inaziba pengo kati ya jadi na mageuzi, inaimarisha maarifa ya pamoja, inaboresha mbinu za tafsiri ya sheria na kufuatilia maendeleo ya kimataifa katika sheria ya Miliki, bunifu ” ameeleza.
“Sisi kama Mahakama tunajihusisha na sheria hasa pale panapokuwa na migogoro kuhusiana na haki hizo na mpaka sasa maamuzi yetu yameenda WIPO na maamuzi 45 kutoka Mahakama zetu na wametoa baadhi ya muhtasari wa shughuli zao, mfano watu wa BRELA.” ameongea Jaji Mwarija.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa BRELA, Godfrey Nyaisa, amesisitiza mwelekeo chanya wa mahakama katika kubadilisha mwelekeo wa sheria za Miliki bunifu nchini, huku akibainisha kuwa Tanzania bado ipo katika hatua ya kujiimarisha kwenye eneo hilo.
Matarajio yetu ni kwamba elimu hii itasaidia kutambua na kulinda bunifu za Watanzania wenzetu kushirikiana na WIPO na ARIPO,” alisema.
Aliongeza pia kwa kusema mashirika hayo yanajulikana kimataifa na duniani kote ambapo ubunifu wowote unaowasilishwa unapitiwa kimataifa na sheria zote zinazotumika zinasaidia kufanya zoezi hilo kikamilifu.
“Tunapojenga uchumi unaotegemea maarifa na kuvutia uwekezaji, umuhimu wa Miliki bunifu katika kuendeleza ubunifu, kuunga mkono utamaduni na kuhakikisha ushindani wa haki hauwezi kupuuzwa,” amesema Nyaisa.
Amebainisha kuwa warsha hiyo imekuja wakati muafaka, ikizingatia mabadiliko ya kimataifa yanayosukumwa na Akili Bandia, biashara za kidijitali na teknolojia zingine mpya, zinazoleta haja ya kuwa na mfumo thabiti na unaojibu changamoto kwa haraka.
Naye, Mkurugenzi wa Utafiti, Muunganiko na Utetezi kutoka Tume ya Ushindani (FCC), Zaitun Kikula, amesema kuwa kwa kushirikiana na WIPO na BRELA, warsha hiyo kwa Majaji wa Rufani ni muhimu katika mchakato mzima wa kulinda Miliki bunifu kulingana na mazingira ya biashara ya nchi.”

