Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga wakati akizungumza na mhandisi wa tume ya madini mkoa wa Rukwa
Picha na Neema Mtuka
…………..
Na Neema Mtuka, Sumbawanga
Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga ameitaka tume ya madini mkoa wa Rukwa kuwasimamia wawekezaji wa ndani na nje ili kuongeza mapato yatokanayo na kodi ya madini hayo.
Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally Chirukile wakati akikagua mgodi wa Acqumarine uliopo Sumbawanga vijijini.
Nyakia amesema kuwa mapato mengi yanapotea kutokana na usimamizi mbovu.
“Tunapoteza madini mengi tena yenye thamani na mnayaacha wanakwepa kodi ninawataka kusimamia ilitusipoteze mapato”
Amesema Nyakia.
Amemtaka mhandisi wa tume ya madini kuhakikisha wana wasimamia wanunuzi wa madini hayo.
Kwa upande wake mhandisi wa tume ya madini mkoa wa Rukwa Liliana Antony amesema kuwa kwa sasa mkoa huo umekuwa ni kivutio kikubwa kwa wawekezaji kwa kuwa milango ya uwekezaji imefunguliwa katika sekta ya madini mbalimbali yanayopatikana katika mkoa wa Rukwa ikiwemo madini ya Acqumarine.
Mhandisi Lilian ameeleza kuwa soko kubwa la madini hayo lipo nchini china ambapo kwa kilo moja wanauza sh 2000 jambo ambalo mkuu wa wilaya ameikataa bei hiyo.
Akitoa taarifa kwa mkuu wa wilaya meneja msimamizi wa uchimbaji wa madini hayo katika kata ya muze wilaya ya Sumbawanga vijijini amesema mpaka sasa wamepata kilo 9 .5 za madini ya Acqumarine ambayo soko kubwa lipo nchini china.
Mkuu huyo wa wilaya amesisitiza juu ya wajibu wa wawekezaji na watumishi kufuata sheria na taratibu zilizowekwa ili pande zote zinufaike na madini hayo.
“Nataka kuona sheria zina zingatiwa hawa wawekezaji wamekuwa wakikwepa kulipa Kodi na kuna baadhi ya watanzania sio wazalendo wanadiliki kusafirisha madini na kuwasaidia wageni kinyume na taratibu zilizowekwa hilo lizingatiwe” amesisitiza nyakia.
Amemtaka meneja msimamizi wa uchimbaji wa madini hayo kuhakikisha wanatunza mazingira na jamii inayozunguka maeneo ya uchimbaji inanufaika na shughuli za uchimbaji katika maeneo hayo.
Baadhi ya wananchi akiwemo Edson mtanga mkazi wa kata ya muze amesema kuwa kuna kasumba kubwa kwa viongozi wachache wa serikali kuwapendelea wawekezaji na wao kuachwa nyuma kwa sababu ya maslahi binafsi.
Madini yanayopatikana katika maeneo tofauti ya mkoa wa Rukwa ni pamoja na madini ya ulanga ,shaba , emerald, titanium,dhahabu,helium,makaa ya mawe na Acqumarine.