Na. WAF, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya imewafikia walengwa wa huduma za chanjo nchini kwa zaidi ya asilima 95 kwa kutekeleza na kuimarisha afua mbalimbali za chanjo.
Hayo yamesemwa na Afisa kutoka Mpango wa Taifa wa Chanjo, Wizara ya Afya, Dkt. Tumaini Haonga wakati wa semina ya waandishi wa habari jijini Dodoma inayoenda sambamba na maadhimisho ya wiki ya chanjo yaliyoanza leo Aprili 24, 2025.
Amesema Tanzania imeendelea kutekeleza utaratibu wa kutoa huduma za chanjo kupitia vituo vya kutolea huduma za afya 8500 vya Serikali na binafsi, kutekeleza huduma mkoba na tembezi ngazi ya jamii na mashuleni pamoja na kushirikiana na Wizara za kisekta ili kutoa huduma hizo mashuleni.
“Kulingana na aina ya chanjo tunayoitoa na walengwa tunaohitaji tunakuwa na mikakati ya kuwafikia wananchi kwa maana ya wazazi, walezi na walengwa husika wa chanjo pale wanapopatikana kwa kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii pamoja na wataalam wa afya kutoka kwenye zahanati zetu na vituo vya kutolea huduma za afya,” amefafanua Dkt. Haonga
Pia ameeleza kuwa utaratibu mwingine unaotumika ni wa kuwatafuta walengwa na kutoa elimu kwa jamii na hatimaye kutoa huduma za chanjo kwa wale ambao hawajapata huduma.
Aidha, Dkt. Haonga ameeleza kuwa hiyo inasaidia kuendelea kuimarisha na kuwa na ufanisi mzuri wa kutoa chanjo na kuhakikisha asilimia tano ya walengwa ambao bado hawajapata chanjo wanafikiwa ili kuweka rekodi nzuri kama Taifa.
Kwa upande wake Afisa Program wa Mpango wa Taifa wa Chanjo Bi. Lotalis Gadau ametoa rai kwa waandishi wa habari nchini kutumia taaluma zao ili kufikisha elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kupata huduma za chanjo za magonjwa mbalimbali hususani chanjo ya Saratani ya Mlango wa kizazi.
“Tulianzisha chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi ni baada ya kuona tatizo limekuwa kubwa hadi hapa tunapoongea takwimu zinaonesha kila mwaka wanawake 10,000,000 wanapata saratani ya mlango wa kizazi, kati ya hao 6,000,000 wanapoteza maisha.
“Wengi wetu hatuna deturi ya kufanya uchunguzi wa saratani hii, hivyo tunajua waandishi wa habari mnasikilizwa hivyo tunaomba mchukue fursa hiyo kupaza sauti kwa jamii ili wapate uelewa kuhusu saratani ya mlango wa kizazi,” amesema Bi. Gadau
Maadhimisho wa wiki ya chanjo hufanyika kila mwaka mwishoni mwa mwezi Aprili ambapo kwa mwaka huu yameanza tarehe 24 hadi 30 Aprili, 2025 yenye kauli mbiu “Chanjo ni Kinga; Tuungane Kuwezesha Walengwa wote Wapate Chanjo”, kilele chake cha maadhimisho haya kitafanyika mkoani Tabora na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama.