MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema hakuna sheria yoyote iliyokiukwa wala kuvunjwa kwa kesi ya Uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu kusikilizwa kwa njia ya mtandao.
“Kesi hii itaendelea kusikilizwa kwa njia ya mtandao ‘video conference’ hadi pale Mahakama itakapoamua yenyewe” kwani sheria ya usikilizwaji wa kesi kwa njia ya mtandao haikuanzishwa kwa sababu ya mlipuko wa ugonjwa wa Covid 19 bali ni sheria iliyotungwa kwa sababu mbalimbali na itaacha kutumika hadi pale itakaposemwa isitumike, hivyo sheria hiyo itatumika wakati wote.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Franco Kiswaga ametoa uamuzi huo leo Aprili 24, 2025 baada ya kusikiliza mabishano makali ya kisheria kutoka pande zote mbili, ule wa Jamuhuri uliokuwa na mawakili watatu wakiongozwa na Nassoro Katuga, Job Mrema na Issa Tawabu huku upande wa utetezi ukiwa na jopo la mawakili zaidi ya 25 wakiongozwa na wakili Mpare Mpoki, Peter Kibatala, Dkt. Lugemeleza Nshala na wenzao.
Mahakama hii ni Committal court. Kifungu cha 148 (1) cha CPA kilitumika Aprili 10,2025 kumpeleka Lissu rumande, lakini hakikutamka mshtakiwa apelekwe gereza gani na kwamba hoja hii imekuwa kandamizi kwa mshatakiwa dhidi ya Magereza ambao hawakuwepo hapa.” Ameseka Kiswaga
Ameendelea kusema kuwa, hoja ya kumuita Mkuu wa Magereza wa Mkoa na Mkuu wa Gereza la Ukonga kuja kuieleza Mahakama kwamba kwa nini mshtakiwa hajaletwa mahakamani? Mahakama inatia shaka kutoa amri hiyo kwa sababu hakuna kifungu kinachoonesha Mahakama kuwaita.
Ameongeza kuwa, siyo lazima Mahakama iombwe, lakini yenyewe inaweza kujiendesha kwa njia ya mtandao, Kanuni ya 10 na Kanuni ya 4 (1) iko wazi, lakini haimaanishi kwamba uamuzi huu utaendelea kuanzia mwanzo wa kesi hadi mwisho, Mahakama kwa badae itaeleza kama itaendelea visual au physical.
Kuhusiana na suala la Mahakama ifanye nini katika suala hilo kwa tarehe zijazo kwamba ifanyike physical ili kila anayetaka kusikiliza asikilize, Hakimu Kiswaga amesema itatolewa link kwa watu wengi wanaweza ili waweze kufuatilia huko huko na kanuni ya 10 haijavunjwa.
“Kesi imeahirishwa hadi Mei 6,2025 saa tatu asubuhi,
Mapema Mawakili wa utetezi Mpoki, Kibatala na Dkt. Nshala waliibua hoja ya kwamba mwenendo wa kesi hiyo ni batili kutokana na sababu mbalimbali.
Miongoni mwa sababu hizo ni kwamba wanaiomba mahakama hiyo isiahirishe kesi hiyo, pia itoe amri kwa Afisa Magereza wa mkoa na Mkuu wa gereza la Ukonga wafike mahakamani kuhojiwa kwamba kwanini mteja wao hajafikishwa mahakamani.
Pia Mahakama itoe tafsiri juu ya kuzuiwa kwa Mawakili na ndugu kumuona Lissu sambamba na mteja wao kuhamishwa gereza bila taratibu kufuatwa
Mbali na hilo, pia upande wa utetezi umehoji kuhusu kesi hiyo kusikilizwa kwa njia ya mtandao ambapo wao wanaomba mteja wao afikishwe mahakamani ili kutoa nafasi kwa watu mbalimbali kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo.
Wamedai Lissu alihamishwa gereza bila mawakili ama mtu yeyote kupewa taarifa na wala hakuwa na uangalizi wowote wa kitabibu na wala hawajui sababu za yeye kuhamishwa, hivyo mahakama ijue kwamba Magereza wamevunja sheria,” amesema Wakili wa Lissu, Jebrah Kambole.
“Tunaiomba mahakama itoe amri kwamba mshtakiwa aachwe azungumze na Mawakili wake pasina kizuizi ikiwemo kuongea naye kwa njia ya simu na kwa kioo, hivyo hakukuwa na usiri baina ya mteja na wakili,” amesema Wakili Nshala.
Hata hivyo, Wakili Peter Kibatala alimueleza hakimu kwamba iingie kwenye rekodi kwamba Lissu alidai hata shiriki katika kesi yake hiyo kwa njia mtandao
Wakijibu hoja hizo, Upande wa Jamhuri waliiomba mahakama itupilie mbali hoja hizo za utetezi.
“Upande wa Jamhuri umeieleza mahakama hii kwamba upelelezi haujakamilika, hii inatoa hitimisho kwamba mahakama yako tukufu inaweza kuahirisha kesi,”
“Kuhusu kuendeshwa kesi kwa njia ya mtandao hiyo ipo kwa mujibu wa kanuni ambapo mahakama hii ina mamlaka bila kuombwa na mtu yoyote kuendesha kesi kimtandao kutokana na sababu mbalimbali,”
“Mwenendo wa shauri la leo ni halali tofauti na kile wanachokisema wenzetu kwamba mahakama hii haiwezi kuahirisha kesi kwa sababu mwenendo huu ni batili,”
Kuhusu hoja za kwamba kuna haki z kikatiba zimevunjwa kwa kesi hiyo kuendeshwa kimtandao, Wakili Katuga alisema kwamba Kisutu sio mahakama ya kikatiba kwa mujibu wa sura ya tatu, marejeo ya mwaka 2019.
Kwa mujibu wa hati ya mahitaka, ilidaiwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam. Ilidaiwa kuwa Lissu akiwa ndani ya jiji la Dar es Salaam alitangeneza nia ya kushawishi au kuchochea umma ya kuweza kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Tanzania kwa kusema maneno yafuatayo;
“Walisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi tutahamasisha uasi, hiyo ndio namna ya kupata mabadiliko….kwa hiyo tunaenda kukinukisha sanasana huu uchaguzi tutaenda kuvuruga kwelikweli, tunaenda kukinukisha vibaya sana.”