Chama cha Madaktari wa Mifugo Tanzania (TVA) kimeandaa Maadhimisho ya Siku ya Tiba ya Mifugo Duniani kwa mwaka 2025, ambayo yatafanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 24 hadi 26 Aprili katika mkoa wa Manyara.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa TVA, Prof. Esron Karimuribo, kilele cha maadhimisho hayo kimepangwa kufanyika Jumamosi, tarehe 26 Aprili 2025, katika Uwanja wa Tanzanite – Kwaraa, mjini Babati.
Maadhimisho haya yamebebwa na kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “Afya ya Mnyama ni Jukumu la Pamoja”, ikiwa ni wito kwa jamii nzima kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha ustawi wa afya ya mifugo nchini.
“Tunawaalika madaktari wa mifugo, wasaidizi wao, wakulima, wafugaji na wananchi wote kwa ujumla kuhudhuria na kushiriki nasi katika maadhimisho haya muhimu. Ni fursa ya kipekee ya kutoa huduma kwa jamii, kubadilishana uzoefu, na kuelimisha umma kuhusu afya ya mifugo,” alisema Prof. Karimuribo.
Katika kipindi chote cha maadhimisho, huduma mbalimbali za afya ya mifugo zitatolewa bila malipo. Huduma hizo ni pamoja na chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo, upasuaji, matibabu ya kitaalamu kwa wanyama, huduma za ugani na elimu kwa umma kuhusu afya ya wanyama.
TVA inasisitiza kuwa afya ya wanyama ni msingi wa maendeleo ya sekta ya mifugo na uchumi wa taifa, hivyo ushirikiano wa wadau wote ni muhimu katika kufanikisha lengo hilo.
Maadhimisho haya yanatarajiwa kuwavutia washiriki kutoka mikoa mbalimbali nchini, yakiwa pia ni jukwaa la kutambua mchango wa madaktari wa mifugo katika ustawi wa jamii na maendeleo ya kilimo na mifugo nchini.