Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Anne Sophie AVÉ, akiwa katika picha ya pamoja na washindi wa pili wa shilingi milioni mbili ambao ni Getrude Malizeni na Natalia Msungu ambao waliibuka washindi katika shindano la picha za michezo.
Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Anne Sophie AVÉ akimkabidhi hundi ya shilingi milioni tatu mshindi wa kwanza wa kupiga picha za michezo lililoongozwa na Ubalozi wa Ufaransa.
Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Anne Sophie AVÉ, akizungumza katika hafla ya kukabidhi zawadi iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo Aprili 24, 2025.
Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
WANAWAKE wawili, Getrude Malizeni na Natalia Msungu, wametajwa kuwa washindi wa pili katika mashindano ya kipekee ya upigaji picha yaliyoandaliwa na Ubalozi wa Ufaransa kwa lengo la kuibua simulizi za wanawake katika ulingo wa michezo hapa nchini. Kwa ubunifu wao na mchango mkubwa waliouonesha kupitia picha, wamezawadiwa kila mmoja shilingi milioni mbili.
Mashindano haya, ambayo yalihusisha wapiga picha wa kike na wa kiume, yalilenga kuonesha kwa kina nafasi ya wanawake kwenye michezo kama judo, rugby, Squash na mpira wa miguu, yakiweka mbele simulizi za mafanikio, ujasiri, na changamoto zinazowakumba wanawake viwanjani.
Mshindi wa kwanza, Jaymes Aloub, alijinyakulia zawadi ya shilingi milioni tatu kwa picha zake zilizogusa hisia na kuonesha ubunifu wa hali ya juu, huku mshindi wa tatu akijinyakulia shilingi milioni moja.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi zawadi iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Anne Sophie AVÉ, amesema:
“Kupitia kamera zao, wapiga picha waliweza kuleta mbele picha zenye nguvu na hadithi ambazo mara nyingi husahaulika – mwanamke akinyanyua uzito, msichana mdogo akijifunza mbinu za rugby, kocha wa kike akiongoza timu yake… Ni picha zinazovunja miiko na kuonyesha kuwa wanawake ni zaidi ya watazamaji wa michezo; wao ni viongozi, wanariadha na vichocheo vya mabadiliko.”
Picha hizo zilishiriki kwenye mitandao ya kijamii ya Ubalozi wa Ufaransa (@franceintanzania) ambapo mashabiki walipewa nafasi ya kupiga kura kwa wiki nne.
Mbali na zawadi ya fedha, washindi pia watajumuishwa katika maonesho maalum ya picha yatakayofanyika kwenye kuta za Ubalozi kama ishara ya kutambua kazi yao ya kuangazia ukweli wa wanawake katika michezo.
Mradi huu ni sehemu ya juhudi za muda mrefu za Ubalozi wa Ufaransa kukuza usawa wa kijinsia na kuimarisha nafasi ya michezo kama chombo cha uwezeshaji wa jamii. Kwa kushirikiana na wadau kama Chama cha Judo cha Tanzania, Weza (Zanzibar), Rugby ya Tucheze na Shule ya Ufaransa.
Mashindano hayo yameonesha kuwa sanaa ya picha inaweza kuwa jukwaa la mabadiliko ya kijamii na chachu ya usawa wa kijinsia.
Kwa kweli, ushindi wa Getrude na Natalia ni ushahidi kuwa wanawake si wa kuangaliwa tu kwenye michezo – ni nguvu inayobeba na kusukuma mbele simulizi za mabadiliko.