Na Said Mwishehe,Michuzi TV- Kongwa
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Stephen Wasira, amesema maana ya demokrasia sio kuhamasisha vurugu na uvunjitu wa amani Bali nii majadiliano, hoja na maelewano kwa lengo la kuimarisha umoja n a ushirikiano nchini, M
Wasira ameeleza hayo leo Aprili 24,2025 alipokuwa wilayani Kongwa mkoani Dodoma akiendelea na ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 ikiwa sehemu ya shughuli za kuelekea maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania ambao uliingiwa Aprili 26, mwaka 1964.
Akieleza zaidi Wasira amefafanua kuwa na demokrasia haina maana ndio naona iwe kwa baadhi ya wanasiasa kuhamasisha vurugu na kuvunja amani, Demokrasia ni kujenga hoja kwa ushawishi wa nguvu ya hoja kwa maslahi mapana ya Taifa ili amani,umoja na mshikamano uendelee kuwepo.
“Kama una hoja za kuwashawishi wapigakura wakukubali toa, kama huna kubali….kwa sababu hawana watu, uchaguzi wa serikali za mitaa wameshindwa kwa sababu hawana wagombea, sasa wanalalamika tumeibiwa mumeibiwa wapi?
“Vijijini humo hawana watu, hata mkienda kwenye kijiji cha Kongwa mkasema niitieni hata watu 10 wa CHADEMA nitakulipa, mtu atapata tabu sana na atakosa hela maana hawapo.
Wasira amesema kutokana na kutokuwa na wananchi wanaowaunga mkono ndiyo maana wapinzani walishindwa kufanya vizuri katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Sasa wewe ukose asiliamia 60 ugombee asilimia 40, uweke watu hawana sifa, ushindwe halafu uende Umoja wa Mataifa, huko utaenda lakini sisi tutakuwa tumeshamaliza hiyo kazi.
Wasira amesema CCM ina ajenda ya kudumu ya kubadili maisha ya watu, yawe mazuri kila mwaka, ya leo yawe mazuri kuliko jana na ya kesho yawe mazuri kuliko ya leo.
Kwa upande wake Spika Mstaafu wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai amesema kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan CCM katika jimbo hilo na mkoa mzima wa Dodoma haina kizingiti cha kushinda uchaguzi mkuu ujao.
Spika Mstaafu Ndugai amesema Kongwa ni kitovu cha uimara wa Chama na kwamba kutokana na kazi nzuri hata uchaguzi ukiitishwa sasa ushindi utapatikana kwa kishindo.
Awali Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene amesema ziara hiyo ya Wasira katika mkoa huo ni ya kiserikali kwa lengo la kuangalia utekelezaji wa ilani na kukagua maendeleo yanayoletwa na serikali ya CCM.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ameeleza katika kipindi cha miaka minne Serikali ya Awamu ya Sita imefanya kazi kubwa hususan kujenga miradi ya maendeleo ambayo inawagusa wananchi moja kwa moja.