Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT)Mkoa wa Ruvuma Rashid Mchekenje kulia,akimpokea Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Simon Chacha ambaye alikuwa Mgeni rasmi kwenye Uchaguzi Mkuu wa Chama hicho uliofanyika katika Ukumbi wa Sky Way Tunduru Mjini,katikati Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Ruvuma Kalemeje Sandali.
Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT)Mkoa wa Ruvuma wakimsikiliza Katibu wa Chama hicho Rashid Mchekenje(hayupo Pichani)alipokuwa akitoa taarifa mbalimbali za kipindi cha miaka mitano kwenye Uchaguzi huo uliofanyika katika Ukumbi wa Sky Way Wilayani Tunduru.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania Mkoa wa Ruvuma Kalemeje Sandali,akizungumza na wawakilishi wa Walimu(hawa Pichani) kutoka Wilaya tano za Mkoa huo kwenye Uchaguzi wa kuwapata Viongozi wapya wa Chama hicho,kulia kwake Mweka hazina Lenzile Mahena na wa pili kushoto Katibu wa Wanawake wa CWT Mkoa wa Ruvuma Lulu Njau.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa ya Chama cha Walimu Tanzania(CWT)anayewakilisha Mkoa wa Ruvuma Sabina Lipukila,akishukuru kwa kupiga magoti baada ya kuchaguliwa tena kushika nafasi hiyo kwa kipindi kingine cha miaka mitano katika Uchaguzi uliofanyika katika kumbi wa Sky Way Mjini Tunduru.
………..
CHAMA cha Walimu Tanzania(CWT)Mkoa wa Ruvuma, kimeiomba Serikali kuangalia upya suala la kikokotoo kwa Walimu kutoka asilimia 40 wanayopokea sasa hadi kufika asilimia 50 ili kuleta ari zaidi ya kazi kwa walimu kufundisha na kukidhi mahitaji yao.
Maombi hayo yametolewa na Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Ruvuma Kalemeja Sandali alipokuwa akizungumza na wawakilishi wa Walimu kutoka Wilaya zote tano za Mkoa wa Ruvuma kwenye Uchaguzi Mkuu wa kuwapata viongozi mbalimbali wa ngazi ya Mkoa uliofanyika katika Ukumbi wa Sky Way Mjini Tunduru.
“Serikali imeongeza kikokotoo kutoka asilimia 35 ya awali hadi asilimia 50, lakini bado haitoshi kutokana na kupanda kwa gharama za maisha,tunaamini Serikali yetu sikivu chini ya Jemedari wetu Rais Samia Suluhu Hassan itatusikiliza na kufanyia kazi”alisema Kalemeje.
Aidha Kalemeje,ameishukuru Serikali kwa kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili walimu hapa nchini ikiwemo mazingira ya kufundishia kwa kujenga na kuboresha miundombinu bora iliyohamasisha walimu kufanya kazi kwa bidii.
Alisema,katika kipindi cha miaka mitano Chama cha Walimu Mkoa wa Ruvuma kimefanikiwa kuanzisha na kusimamia miradi mbalimbali itakayowakwamua walimu na Chama kiuchumi ikiwemo kununua mabasi ambayo yamesaidia kurahisha safari za walimu wanapokwenda kwenye ziara za mafunzo.
Mchekenje alisema, katika kipindi cha miaka mitano 2025-2030 Chama kitafanya usajili ili kuhakikisha shule zote za Msingi na Sekondari pamoja na taasisi nyingine za elimu zinatembelewa ili walimu waliopo kazini na wale wa ajira mpya wanakuwa Wanachama na kuchangia michango ya asilimia 2 kwa Chama hicho.
Kwa mujibu wa Mchekenje,watahakikisha Wanachama wastaafu walioko Wilayani wanatambuliwa na kuorodheshwa ili kupata wepesi wa ulipwaji mkono wa kwaheri unafanyika kwa wakati,kufuatilia na kuzingatia ufumbuzi wa kero za wanachama ikiwemo madai mbalimbali,madaraja,posho,uhamisho na matibabu.
Pia alisema,katika kipindi cha miaka mitano iliyopita mapato ya Chama ni Sh.568,671,345.91 na salio anzia lilikuwa Sh.71,466.68 hivyo jumla ya mapato kuwa Sh.milioni 568,742,812.59 ambazo zilitoka kwenye vyanzo mbalimbali ikiwemo marejesho ya asilimia 8,pango la Jengo la Chama.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa wa Chama hicho anayewakilisha Mkoa wa Ruvuma Sabina Lipukila alisema,katika kipindi cha miaka mitano atashirikiana na Serikali ya Mkoa na Taifa kuhakikisha changamoto za walimu zinapatiwa ufumbuzi ili walimu wapate mazingira bora ya kazi.
Lipukila ambaye amechaguliwa kushika nafasi hiyo katika kipindi kingine cha miaka mitano,amewataka walimu kufanya kazi kwa bidii ili waweze kupata matokeo mazuri ambayo yataleta tija katika Mkoa wa Ruvuma na kuwa na miongoni mwa Mikoa inayofanya vizuri kwenye matokeo ya mitihani ya Kikanda na Kitaifa.
Akifungua Mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Simon Chacha,amekipongeza Chama cha Walimu Mkoa wa Ruvuma kwa kufuata Katiba yao inayowataka kufanya Uchaguzi wa Viongozi wake kila baada ya miaka mitano.
Chacha,amempongeza Rais Samia Suluh Hassan na Serikai yake ya awamu ya sita kwa jitihada kubwa inayofanya kwa kuboresha miundombinu ya elimu na mazingira ya kazi kwa walimu hapa nchini.
Amewahakikishia Walimu wa Mkoa wa Ruvuma kwamba,Serikali inaendelea kutekeleza na kufanyia kazi changamoto mbalimbali zinazowakabili Walimu ikiwemo madai ya posho.