Katika kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ally Mwinyi, ameweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Kibada – Mwasonga – Kimbiji yenye urefu wa kilometa 41, hatua muhimu inayolenga kukuza uchumi na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo Aprili 25, 2025, katika Wilaya ya Kigamboni, Dkt. Mwinyi alisisitiza kuwa uwepo wa amani nchini ndiyo msingi wa mafanikio ya miradi ya maendeleo kama huu, na kuagiza ujenzi huo ukamilike kwa wakati na kwa viwango vya juu. Alibainisha kuwa barabara hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali kuunganisha maeneo ya pembezoni na fursa za kiuchumi.
Katika hotuba yake, Dkt. Mwinyi alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuendeleza Muungano na kutatua changamoto zilizokuwa zikikumba uhusiano kati ya pande mbili za Muungano, akisisitiza kuwa umoja huo ni nguzo ya maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, aliyemwakilisha Waziri wa Ujenzi, alisema mradi wa barabara hiyo ni jawabu kwa kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Kigamboni, na sasa utafungua fursa za uwekezaji na kuinua uchumi wa eneo hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, alimhakikishia Rais Mwinyi kuwa Mkoa upo salama na utazidi kudumisha amani licha ya changamoto za kisiasa, huku akitoa pongezi kwa Rais Samia kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi ya kimkakati kama hii.
Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Muhammed Besta, alieleza kuwa barabara hiyo inajengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 83.8 na itatekelezwa kwa awamu mbili chini ya mkandarasi kampuni ya Estim, ambapo hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 30.
Uzinduzi wa mradi huu umebeba ujumbe mzito wa kaulimbiu ya mwaka huu isemayo: “Muungano wetu, heshima na tunu ya Taifa – Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025”, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya Muungano.