Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Tanzania, Dkt. Mustapher Siyani, amepongeza ushirikiano unaondelea baina ya Muhimili wa Mahakama na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ambao umeelezwa kuwa ni muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hizo mbili za serikali.
Ametoa pongezi hizo wakati akifungua mafunzo kwa Watendaji wa Mahakama Kanda ya Kati yaliyobeba Kauli Mbiu isemayo: Nafasi ya Teknolojia na Akili Unde Mahali pa Kazi (Fursa na Mapinduzi) ambayo yameandaliwa na OSHA kwakushirikiana na Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi na kuwezeshwa na OSHA.
Mafunzo hayo yenye washiriki zaidi ya 100 yamefanyika katika Ukumbi wa OSHA Dodoma kwa siku mbili mfulizo (Aprili 23-24, 2025), yakiwahusisha watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kati wakiwemo Majaji Wafawadhi, Majaji, Wasajili, Manaibu Wasajili, Mahakimu, Watendaji wa Mahakama na Wasaidizi wa Majaji.
Katika hotuba yake Jaji Siyani amesema: “Niwashukuru OSHA kwa kuendelea kuwezesha mafunzo ya watumishi wa Mahakama kwani kwa kumbukumbu zangu mwezi Disemba mwaka jana tulikutana katika ukumbi huu kwa mafunzo kama haya.
Hivyo, mwendelezo wa mafunzo haya ni jambo la kuigwa na Taasisi nyingine,” ameeleza Jaji Kiongozi.
Aidha, amesema mafunzo hayo ni muhimu sana kwa washiriki ambao ni wadau wa utoaji haki na huduma katika sekta mbalimbali hasa kwa kuzingatia maudhui ya mafunzo hayo ambayo yamejumuisha mada mbalimbali zikiwemo sheria mbalimbali za ndani na nje ya nchi, Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi pamoja na matumizi ya Akili Unde.
Aidha, ameeleza kuwa matumizi ya akili unde yameonesha mafanikio katika nchi mbalimbali duniani hivyo ni muhimu kwa Tanzania kuanza kujiandaa na matumizi ya teknolojia hiyo hususan katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali yakiwemo ya Mahakama kwakuwa Tanzania sio kisiwa.
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Dkt. Yose Mlyambina, amesema Mahakama Kuu wanajivunia uhusiano uliopo baina yao na OSHA ambao umeendelea kukua siku hadi siku na hivyo kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wa haki kazi.
Akitoa salama zake katika ufunguzi wa mafunzo husika, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema mafunzo hayo yanafaida mara mbili kwa Watendaji wa Mahakama kwakuwa yanawapa uelewa wa masuala ya usalama na afya wakiwa kama wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kuijua Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi jambo ambalo linaweza kusaidia katika kushughulikia kesi zinazohusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.
Mafunzo haya ni ya awamu ya pili baada ya awamu ya mafunzo ya awamu ya kwanza yaliyokuwa yanahusu Usalama Afya, Haki na Wajibu kwa Watu wenye Ulemavu yaliyofanyika Disemba 16 hadi 17, 2024.
