


NA BALTAZAR MASHAKA, MAGU
Halmashauri ya Wilaya ya Magu imepata mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hadi kufikia mwaka 2024/25 mapato ya ndani yameongezeka kutoka sh. bilioni 2.4 mwaka 2021 hadi kufikia bilioni 5.2 kwa mwaka.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,Mpandaule Simon,amesema leo wakati wa kikao cha robo ya tatu cha Baraza la Madiwani, ambapo alieleza kuwa ongezeko hilo la mapato limechochea utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kimkakati, hususan katika sekta ya elimu na afya.
Amesema walipoingia madarakani mwaka 2020/21, kulikuwa na udhaifu mkubwa uliosababisha halmashauri kukusanya sh.bilioni 2.4 za mapato ya ndani,lakini kutokana na mikakati na usimamizi mzuri wa makusanyo katika vyanzo, mwaka uliofuata walikusanya sh.bilioni 3.6 na baadaye bilioni 3.8.
Simon amesema udhibiti wa ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha za miradi uliiwezesha Halmashauri ya Magu, kukusanya sh.bilioni 5.2 ambapo kwa miaka minne mfululizo imepata hati safi baada ya taarifa ya ukaguzi ya CAG.
“Haikuwa kazi rahisi eneo la mapato ya ndani,tuliweka mkakati wa makusanyo tukiwahusisha watendaji wa wa kata, leo tunakusanya bilioni 5.2 ambapo asilimia 40 ya mapato yetu hayo yametumika kujenga shule 24 za sekondari na shule 11 za msingi katika maeneo mbalimbali ya wilaya,” amesema na kuongeza.
“Ni jambo la kujivunia na ni hatua kubwa ya kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya elimu bora na katika mazingira mazuri,.amoja na kupigwa vita na fitina za kisiasa,madiwani tumefanya kazi kubwa ya kuwatumikia wananchi, binafsi ninayo furaha kubwa sijawaangusha wana Magu.”.
Simon amesema katika sekta ya afya, halmashauri hiyo imefanikiwa kuboresha Kituo cha Afya cha Nyanguge kwa sh. milioni 100, hatua inayolenga kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa maeneo ya jirani, kwamba kazi kubwa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya imefanyika kwa weledi kwa kodi zao pia, kurudisha fadhila kwa kura zao.
Amesema kwa miaka mitano wameimarisha usimamizi wa mapato,wameibua vyanzo vipya ikiwemo stendi ya Kona ya Kayenze,stendi ya zamani inaingiza milioni 31 badala ya milioni 14 huku madini ujenzi yakiingizia halmashauri sh.milioni 54 hadi 60 kutoka sh. milioni 22 kwa mwaka.
Mwenyekiti huyo wa Halmashauri na Diwani wa Nyigogo (CCM) ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiunga mkono halmashauri hiyo kwa vitendo .
Naye Diwani wa Sukuma (CCM), Faustine Makingi amesema serikali kuu imejenga shule ya wasichana ya sekondari ya Magu Girls yenye hadhi ya kisasa kwa sh. bilioni 3, sambamba na kuleta zaidi ya sh.milioni 850 kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili mpya za msingi.
“Tumepiga hatua kubwa katika sekta ya elimu tumepandisha ufaulu na hakuna sifuri.Afya huduma zimesogezwa karibu na wananchi, tunamshukuru Rais wetu kwa moyo wake wa kuwekeza katika maendeleo ya wananchi, hasa kwenye elimu na afya. Haya ni mafanikio makubwa ambayo kila mwananchi wa Magu anapaswa kujivunia,” ameongeza.
Kwa mujibu wa Diwani wa Viti Maalum, Stella Anthony, mafanikio hayo ukiemo ujenzi wwa zahanati saba ni kielelezo cha usimamizi bora wa rasilimali, uwazi katika matumizi ya fedha za umma, na ushirikiano mzuri kati ya viongozi wa halmashauri na wananchi.