Na Silivia Amandius.
Kyerwa, Kagera.
Wilaya ya Kyerwa, Mkoa wa Kagera – Mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 15 kati ya ndugu wawili wa familia ya Mfuruki umefikia tamati kwa mafanikio kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.
Bi. Generoza Mfuruki na kaka yake, Bw. Idrisa Mfuruki, walikuwa katika mvutano kuhusu umiliki wa shamba lenye ukubwa wa ekari 20 lililoachwa na baba yao mzazi, Bw. Mfuruki. Chanzo cha mgogoro kilianza wakati baba yao alipougua, ambapo Bi. Generoza aliuza nusu ya shamba hilo kwa kaka yake ili kusaidia gharama za matibabu. Hata hivyo, baada ya kifo cha baba yao, Bw. Idrisa alidai umiliki wa eneo lote, jambo ambalo lilipingwa na Bi. Generoza, akisisitiza kuwa nusu ya shamba bado ni mali yake.
Bi. Generoza na Bw. Idrisa ndugu hao wameeleza furaha yao kwa kupatiwa elimu na usurihishi wa amani baina yao kauhakikisha wanamaliza tofauti zao zilizokuwepo kati yao na kumshukuru mh. Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suruhu Hassan na kuomba uwepo endelevu wa kampeini hiyo kwani inaenda kuwa mwangaza hata kwa wananchi wengine.
Kupitia juhudi za timu ya msaada wa kisheria ya mama Samia Usuluhishi ulifanyika mbele ya viongozi wa kata kyerwa kijiji kagenyi ambapo Bi. Generoza alikubali kuuza nusu ya shamba lililokuwa limebaki kwa kaka yake kwa kiasi cha shilingi milioni 2 na Bw. Idrisa alikubali kulipa fedha hizo katika kipindi cha msimu wa kahawa Julai mwaka huu.
Nae Wakili wa serikali kutoka halmashauri ya wilaya ya kyerwa ndg. Eliah Shadewa ambae alikuwa sehemu ya timu ya usuluhishi alieleza kuwa wananchi wengi wanaingia kwenye migogoro kutokana na ukosefu wa uelewa wa sheria na taratibu za mirathi, alisisitiza kupitia kampeini hiyo wananchi wamepata elimu ya kisheria ambayo itawasaidia kuepuka migogoro ya aina hii katika siku zijazo.
Kupitia kampeni hii, wananchi wanapatiwa msaada wa kisheria bure unaolenga kuwasaidia kutatua migogoro ya ardhi kwa njia ya haki na kikatiba. Hii inafanyika kwa kutoa elimu ya kisheria, kusaidia wananchi kuelewa haki zao za kikatiba, na kuwasaidia kufuata taratibu sahihi za kisheria ili kuepuka migogoro ambapo kampeini hii imefanikiwa kuwafikia wananchi zaidi ya milioni 1.3 mpaka sasa na kushughulikia migogoro mingi kisheria nchini.