Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ametoa maelekezo kwa Wizara ya Maji kuweka msukumo na kipaumbele ili mradi wa maji wa Tarime – Rorya ukamilike kwa wakati uliopangwa na wananchi waone matunda yake.
Balozi Nchimbi amesema mradi huo ni mojawapo ya miradi ya maji mikubwa nchini ambayo inalenga kutatua tatizo kwa muda mrefu ujao, hivyo akahimiza uwekewe msukumo ili wananchi wanaolengwa waanze kuona maji yakitoka.
Mradi huo ulioko katika eneo la Mogabiri, Tarime Vijijini, wenye gharama ya Tsh. 134 bilioni, unatarajiwa kuhudumia jumla ya wakazi wapatao 729,496, ukiwa umesanifiwa kwa ajili ya kumaliza changamoto ya maji katika maeneo ya wilaya za Tarime, Rorya na Serengeti.
Balozi Nchimbi aliipongeza Serikali ya CCM, chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa jinsi ambavyo imeupatia uzito mradi huo kwa kuhakikisha mkandarasi analipwa malipo yake yote hadi hatua aliyofikia sasa.
Katibu Mkuu huyo wa CCM pia aliipongeza Wizara ya Maji, wataalamu na wahusika wote waliosanifu mradi wenye tija, huku pia akiipongeza Serikali mkoani Mara, CCM Mkoa wa Mara, wabunge wa maeneo hayo na Baraza la Halmashauri kwa kusemea na kusimamia mradi huo muhimu.