Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa Mgodi wa North Mara kwenye maonesho ya kimataifa ya Afya na Usalama mahali pa kazi , yanayoratibiwa na Wakala wa Afya na Usalama wa Mahali pa kazi (OSHA) yanayofanyika viwanja vya Mandewa mjini Singida
Afisa wa Mgodi wa Bulyanhulu , akitoa ufafauzi wa Mkuu wa Mkoa wa Singida , Mhe. Halima Dendego kwenye maonesho ya afya na usalama mahali pa kazi viwanja vya Mandewa mjini Singida
Chrisant Madubu , Mkufunzi wa Mafunzo na Usalama wa Mgodi wa Bulyanhulu akitoa ufafanuzi wa jinsi mgodi huo unavyotekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya Akili Mnemba kwa ajili ya usalama wa wafanyakazi wake kwenye maonesho ya usalama mahali pa kazi viwanja vya Mandewa mjini Singida
Mrakibu Mwandamizi wa Usalama wa Mgodi wa North Mara, Bw. Meshack Issack akitoa maelezo na ufafanuzi kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida , Bi Halima Dendego kuhusu vifaa na mitambo inavyofanya kazi kwenye maonesho ya usalama na afya mahali pa kazi mjini Singida
****
Migodi ya Barrick na Twiga ya Bulyanhulu, North Mara na Buzwagi inadhihirisha kwa vitendo kauli mbiu ya wiki ya maadhimisho ya wiki ya kimataifa ya OSHA nchini mwaka huu isemayo nafasi ya Akili Mnemba na Teknolojia katika kuimarisha Afya na Usalama kazini kutokana na kuwekeza katika matumizi ta teknolojia za kisasa za kimataifa katika uendeshaji wa shughuli zake.
Katika Maonesho ya Afya na Usalama mahali pa kazi ambayo hufanyika kila mwaka na kuandaliwa na Wakala wa Afya na Usalama na mahali pa kazi (OSHA) yanayofanyika katika viwanja wa Mandewa mjini Singida wananchi wengi na viongozi mbalimbali wanatembelea banda la maonesho la migodi ya Barrick na kujionea teknolojia za kisasa za kidigitali za kudhibiti majanga na kupata mafunzo ya kuhusiana na usalama mahali pa kazi na kwenye jamii.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego alipotembelea Banda la mgodi wa Barrick yenye ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga, amesema kwamba mitambo , magari ya kisasa, vifaa vya tekonolojia na kidigitali ni chachu ya mabadiliko ya utendaji kazi kwenye sekta ya uchimbaji wa madini kama ambavyo migodi ya Barrick inaendesha shughuli zake.
“Kwa kweli kwa matumizi ya digitali na akili mnemba migodi ya Barrick mnafanya vizuri katika kuhakikisha usalama wa wafanyakazi pamoja na jamii inayozunguka migodi , hili ni jambo la kuungwa mkono kwa dhati na kuigwa na makampuni mengine katika sekta ya uchimbaji madini,” amesema Mhe. Dendego.
Aliongeza kwamba ni muhimu kwa kuhakikisha usalama na afya za wafanyakazi kama vile migodi ya Bulyanhulu , Buzwagi na North Mara inavyowekeza katika teknolojia za kisasa ili kudhibiti madhara yatokanayo na ajali na majanga mengine kwenye sekta ya madini.
Akitoa ufafanuzi kwa Mkuu wa Mkoa huyo, Mrakibu Mwandamizi wa Usalama, Bw. Meshack Issack kutoka Mgodi wa North Mara, amesema mgodi huo unatumia mitambo ya kisasa ya uchimbaji wa dhahabu chini ya ardhi na kuachana na matumizi ya binadamu katika uchimbaji wa dhahabu chini ya ardhi hali ambayo inaleta Usalama na afya kwa Wafanyakazi.
“Tuna mashine za kisasa za teknolojia ya kimataifa (automation) ambazo zinaendeshwa na mfanyakazi akiwa ofisini lakini anachimba dhahabu chini ya ardhi ambayo inaweza kutambua hali hatarishi yoyote kwenye miamba na kuta za chini ya ardhi,”ameeleza.
Ameongeza kwamba kwa mgodi huo umeachana uchimbaji wa kizamani kwa kutumia akili mnemba ambao inarahisisha kazi na kuokoa muda na mfanyakazi wa mitambo hiyo ya kisasa anatumia rimoti katika ufanyaji wake wa kazi.
Kwa upande wake , kiongozi wa Usalama na Afya wa Mgodi wa Buzwagi , Dkt. Ludovick Sirima, amesema kwamba mgodi huo upo kwenye hatua za ufungaji baada ya shughuli za uchimbaji dhahabu kuisha lakini afya na usalama wa wafanyakazi ni kipaumbele chao.
“Pamoja na mambo mengine Mgodi wa Buzwagi unaendelea na jitihada za kuandaa kongani maalum la uwekezaji ili kuhakikisha baada ya shughuli za ufugaji kuisha basi watanzania wanapata fursa nyingine ya kibiashara na uwekezaji wa kuzingatia usalama na afya mahali pa kazi,” amesisitiza Dkt. Sirima.
Chrisant Madubu , Mkufunzi wa Mafunzo na Usalama wa Mgodi wa Bulyanhulu amesema mgodi huo unatekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya akili mnemba mahali pa kazi kwa kuachana na matumizi ya karatasi na kuweka mifumo ya teknolojia na kidigitali kwa kuwa na mitambo na magari ya kisasa katika shughuli za uchimbaji.
“Kampeni yetu ya ‘Journey to Zero’ inalenga kuhakikisha Wafanyakazi wote wa kampuni wanakuwa salama wakati wote wanapokuwa kazini hadi wanaporudi nyumbani na tumehakikisha kampeni hii inavuka mipaka hadi nje ya kampuni kuhakikisha jamii nzima inakuwa salama ndio maana tunaendelea kutoa mafunzo ya usalama kwa jamii”,amesema.
Mmoja wa wageni waliotembea mabanda ya migodi ya Barrick,John Lucas mkazi wa Iyambi Singida, amesema amevutiwa jinsi mgodi unavyotekeleza sera ya Afya na usalama sambamba na matumizi ya vifaa vya kisasa katika kudhibiti majanga.
“Usalama ni jambo la msingi ni muhimu nasi wananchi tupatiwe elimu ya kukabiliana na majanga ili tubaki salama katika jamii”,amesema.