MKUU wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego amelipongeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa utekelezaji wa majukumu yake ya kuhakikisha Sekta ya usafiri majini inachangia kukuza Uchumi wa Taifa.
Ametoa pongezi hizo wakati alipotembelea Banda la TASAC, leo tarehe 26 Aprili,2025 katika Maonesho ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) yanayofanyika katika Viwanja vya Mandewa mkoani Singida.
“Sekta ya usafiri majini inakua kwa kasi sana, hivyo natoa rai kwa TASAC kuendelea kusimamia sekta hii ili iweze kuleta mabadiliko katika nchi,” amesema Mhe. Dendego.
Akiwa katika banda hilo Mhe. Dendego alipata maelezo kutoka kwa Afisa Uhusiano Mwandamizi, Bi. Mariam Mwayela kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na TASAC ikiwemo kudhibiti na kusimamia usalama, ulinzi wa vyombo vya usafiri na utunzaji wa mazingira majini; udhibiti wa huduma za usafiri majini pamoja na kutoa huduma ya uwakala wa forodha kwa bidhaa mahsusi kwa mujibu wa Sheria.
“Sisi kama TASAC tumekasimiwa majukumu ya kudhibiti na kusimamia usalama, ulinzi na utunzaji wa mazingira ya vyombo vya usafiri majini na kuhakikisha vyombo, abiria na mizigo vinakua salama lakini pia kwa kuzingatia miongozo ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi kuhakikisha watumishi wote wanakuwa katika hali ya usalama katika mazingira wanayofanyia kazi,” amesema Bi. Mwayela.
Katika maonesho hayo, wadau mbalimbali wametembelea Banda la TASAC akiwemo Mwenyekiti wa TUICO Taifa Bw. Paul Sangeze.
TASAC ni moja ya taasisi zinazoshiriki Maonesho ya Kimataifa ya OSHA yenye kauli mbiu “ Nafasi ya Akili Mnemba na Teknolojia za Kidijitali katika kuimarisha Usalama na Afya Mahali Pa Kazi”.
Maonesho haya yanatarajiwa kufikia kilele mnamo tarehe 30 Aprili, 2025.