*Utafiti wafanyika katika visima vinne
*Utafiti umegundua gesi ya Helium yenye ubora wa mkusanyiko wa asilimia 7.9 na 5.5
*Zaidi ya ajira 100 zatolewa kwa jamii
Momba, Songwe.
Imeelezwa kwamba utafiti wa gesi ya helium uliofanywa na kampuni ya HeliumOne nchini Tanzania umefanikiwa kupata gesi hiyo katika umbali wa kilomita 1.14 kutoka chini ya ardhi katika visima vya Itumbula West 1 na Tai 3.
Msimamizi wa mradi huo Emmanuel Ghachocha alibainisha kwamba, majibu ya utafiti katika kisima cha Itumbula West 1 yalionesha kuwa na wingi wa mkusanyiko wa gesi ya helium juu ya kisima yenye ubora wa kiwango cha asilimia 7.9 jambo lililoleta matumaini ya kuendelea na utafiti wa kina.
Ghachocha alifafanua kuwa, utafiti wa kina (Extended Well Test) ulionesha uwepo wa mkusanyiko wa gesi hiyo kwa kiwango cha asilimia 5.5 iliyopanda juu ya ardhi kutoka kisima cha Itumbula West1 ambayo ubora wake ni mzuri kulingana na majibu ya sampuli zilizochunguzwa katika maabara mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Akielezea kuhusu matumizi ya teknolojia katika utafiti hususan katika utumiaji wa mashine za kisasa kwenye utafiti Ghachocha alisema kuwa, kampuni ya Helium One ilifanikiwa kununua mitambo yake yenyewe ikiwamo winchi za unyanyuaji vifaa pamoja na mtambo wa uchimbaji (Predator drilling rig) jambo ambalo limeongeza ufanisi katika kipindi cha utekelezaji wa utafiti huo.
Kuhusu Mpango wa Wajibu wa Kampuni kwa Jamii inayozunguka Mgodi (CSR) Ghachocha alisema kuwa, mpaka sasa kampuni imetoa ajira za kudumu na zisizo za kudumu zaidi ya 100 zimetolewa na kampuni kwa jamii inayozunguka mgodi na nje ya mgodi.
Sambamba na hapo mwaka 2021/2022 kampuni ilichangia zaidi ya milioni 50 katika maboresho ya shule za Kata ya Itumbula, Mpapa, Mkulwe na Ivuna.
Mwaka 2023 kiasi cha shilingi milioni 54 zilitolewa na heliumOne katika kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Mkonko na kutoa msaada wa vifaa tiba na samani za zaidi ya takribani shilingi milioni 20 kwa ajili ya zahanati hiyo na kituo cha afya cha Kamsamba. Pia takribani shilingi milioni 15 zilitolewa kwa jamii ya Itumbula iliyopata madhara ya kimbunga.
Itakumbukwa kwamba kampuni ya HeliumOne iliwasilisha maombi ya leseni ya madini kwa ajili ya eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 480 lililojumuisha Bonde la Rukwa Kusini , mwezi Machi 2025 Helium One ilikubali rasmi ofa ya leseni hiyo kutoka Wizara ya Madini kwa hatua za utekelezaji wa uzalishaji wa gesi hiyo nchini.