


Happy Lazaro, Arusha
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko amezindua mradi wa upanuzi wa kituo cha kupooza umeme cha Njiro Arusha.
Aidha mradi huo wa upanuzi wa kituo cha kupooza umeme cha Njiro Arusha wa kuongeza transfoma yenye uwezo wa MVA 90 na kufanya kituo kuwa na uwezo wa MVA 210 .
Akitoa maelezo kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa nishati Dkt.kuhusu mradi huo ,Meneja mradi huo ,Jaffari Msuya amesema kuwa , mradi huo umeanza ramsi mwaka 2023 na kumalizika 2025.
Amesema uwepo wa mradi huo utasaidia sana kuongeza upatikanaji wa umeme kanda ya kaskazini ikiwemo mkoa wa Arusha ,Tanga na Kilimanjaro na hayo ni manufaa makubwa sana kwa wananchi wetu.
“Mradi huu uko chini ya wizara ya Nishati kupitia Tanesco na umetekelezwa na fedha za ndani .”amesema Msuya.
Akizungumza na wananchi katika hafla za Sherehe za muungano wa Tanganyika na Zanzibar Mkoani Arusha, mara baada ya kuzindua kituo hicho ,Dkt Biteko amesema kuwa Serikali imetumia kiasi cha Shilingi Bilioni 5.2 kwa ajili ya upanuzi wa Kituo hicho ili kukiongezea Kituo uwezo kuendana na ongezeko la matumizi ya umeme.
“Katika ukanda huu, mahitaji ya umeme kwenye Mkoa wa Arusha ni megawati 107, Tanga Megawati 126, Manyara Megawati 14, na Kilimanjaro Megawati 68, na leo tumezindua upanuzi wa Kituo cha kupoza umeme cha Njiro, ambacho kina njia kumi za kusambaza umeme katika Mkoa wa Arusha na kuuwezesha Mkoa huu kukidhi mahitaji ya umeme kufikia Megawati 200 kulinganisha na mahitaji ya sasa ambayo ni Megawati 107” amesema Mhe. Dkt. Biteko
Aidha Mhe. DKt. Biteko amesema kuwa Serikali ipo kwenye mpango wa utekelezaji wa kufanya maboresho ya miundombinu ya umeme ikiwa ni maagizo ya Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha miundombinu ya umeme chakavu yote inafanyiwa ukarabati wa njia za kusafirisha umeme.
“Umeme tunaweza kuwa nao kwenye uzalishaji, lakini ikawa changamoto kwenye miundombinu, ndio maana Mhe. Rais ametuagiza sasa kufanya maboresho ya miundombinu ya umeme ili tuwe na umeme wa uhakika, alisema Mhe. Dkt. Biteko.
Ameongeza kwa kusema kuwa Wizara ya Nishati imekusudia kuhakikisha kila Mtanzania anapata kipande cha keki ya Nishati hasa Nishati ya umeme.
Nilipoteuliwa niliwaambia, TANESCO hamtalala usingizi, na wote mnashuhudia kuwa hali ya umeme imebadilika sio kama miaka kumi nyuma, na TANESCO kwa kweli hawalali wanafanya kazi nzuri” alisema Mhe. Dkt. Biteko.
Kukamilika kwa Kituo hicho kutaimarisha hali ya upatikanaji wa umeme kwenye Mikoa ya Kanda ya Kaskazini ikiwemo Mkoa wa Arusha na kuifungua kiuchumi kwa kukuza Sekta za Utalii, Viwanda na Biashara.
Naye Mkandarasi wa mradi huo,Mao Bo kutoka kampuni ya Xian Electric Engineering Co.Ltd ambao ndio watekelezaji wa mradi huo amesema kuwa mradi huo umekamilika kwa wakati na kukamilika kwake utaleta manufaa makubwa sana kwa wananchi kutokana na kuongezeka kwa umeme wa kutosha.
Amesema kuwa, tayari wananchi wameshaanza kunufaika na umeme huo hususani wananchi wa kanda ya kaskazini na kutosheleza mkoa wa Arusha.
“Hapo awali kulikuwa na changamoto ya uwezo mdogo wa upatikanaji wa umeme ila kutokana na mradi huu wananchi wataweza kupata umeme wa kutosha na wa uhakika.”amesema