
Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Dkt Damas Suta katikati,akizungumza na baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Dkt Samia Suluhu Hassan(hawapo pichani)baada ya kukagua maonyesho ya Kisayansi wakati wa mahafali ya kwanza ya kidato cha sita,kushoto Mkuu wa Shule hiyo Dafrosa Chilumba.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Dkt Samia Suluhu Hassan iliyopo Wlaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Dafrosa Chilumba,akizunguza na Wanafunzi,Walimu,Wazazi na Wageni waliofika kwenye mahafali ya kwanza ya kidato cha Sita yaliyofanyika jana ambapo jumla ya Wanafunzi 204 wanatarajia kuhitimu masomo yao.

Baadhi ya Wahitimu wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Dkt Samia Suluhu Hassan,wakiwa kwenye maandamano kabla ya kufanyika kwa mahafali ya kwanza ya kidato cha sita jana.
………
SHULE ya Sekondari Dkt Samia Suluhu Hassan iliyopo Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma,imefanya mahafali ya kwanza ya kidato cha sita ambapo jumla ya wanafunzi 204 wanatarajia kuhitimu masomo yao mwaka 2025.
Akizungumza wakati wa mahafali hayo mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Dkt Damas Suta,amewapongeza wanafunzi wote wa kidato cha sita kwa kumaliza rasmi safari yao ya elimu ya Sekondari na kuonyesha nidhamu,bidii na ustahimilivu mkubwa katika maisha yao ya kielimu na kimaendeleo.
Dkt Suta,amewataka wahitimu hao kutambua kuwa,mahafali hayo sio mwisho wa safari yao kielimu,bali yawe chachu ya kuendelea mbele kwa kuwa Dunia ya sasa inahitaji watu walioelimika,wabunifu na wenye maadili mema.
“Mtakapoondoka hapa kumbukeni kuwa bado mna jukumu kubwa kwa jamii inayowazunguka na Taifa kwa ujumla,jiwekeni tayari kwa hatua inayofuata iwe kwa ajili ya kujiunga na elimu ya juu au kunzisha shughuli za kujitegemea,mkatumie mitandao ya kijamii kwa ajili ya maendeleo yenu,Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla”alisema Suta.
Aidha,amewataka Wazazi na walezi Mkoani Ruvuma kuhakikisha wanapeleka watoto shule ili wapate haki yao ya msingi na kufuatilia mienendo yao ili kuepuka kwenda kinyume na maadili na utamaduni wa nchi yetu.
Sambamba na hayo,amewaasa Wanafunzi wanaobaki kutokata tamaa,kuogopa changamoto badala yake wahakikishe wanazingatia masomo ili maisha yao ya shule yawe na tija kitaaluma,kinidhamu na vipawa mbalimbali.
Suta,amewapongeza Walimu kwa kazi kubwa na ya kipekee waliyofanya kwani mafanikio ya wanafunzi wa shule hiyo ni ushahidi wa juhudi zao,maarifa na moyo wa kujitolea ambayo ni nguzo muhimu katika ujenzi wa Taifa letu na wazazi kwa kulea,kusaidia na kuwahimiza watoto wao hadi kufikiwa hatua hiyo.
“Bila ushirikiano wa Wazazi,mafanikio haya yasingepatikana,mmefanya kazi kubwa,lakini tunawaomba mzidi kuonesha ushirikiano mkubwa zaidi katika kuwahudumia wanafunzi mahitaji yao ya lazima ya kitaaluma ili waweze kutimiza ndoto zao”alisema Suta.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule hiyo Dafrosa Chilumba alisema,Shule ya Sekondari ya Wasichana Dkt Samia Suluhu Hassan ilianza kujengwa mwaka 2022 na kukamilika mwaka 2023 na ni Shule jumuishi inayochukua wanafunzi na wenye mahitaji maalum kuanzia kidato cha kwanza hadi sita na ina jumla ya Wanafunzi 676.
Kwa mujibu wa Chilumba,Shule ya Dkt Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa shule mpya za Wasichana za Mikoa zilizoanzishwa na Serikali ya awamu ya sita kwa dhamira ya kuimarisha elimu ya Sekondari kwa Wasichana kupitia mradi wa kuimarisha elimu ya Sekondari Nchini (SEQUIP).
Alisema,wahitimu wanaotarajiwa kuhitimu kidato cha sita mwaka huu,wanafunzi 43 kwa tahasusi ya PCB,44 CBG,37 HGL,39 HGK na Wanafunzi 41 tahasusi ya HKL.
Chilumba,ameishukuru Serikali kwa kutoa Sh.bilioni 4.450 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya kisasa ya Wasichana ambayo itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 1,200 na hiyo ni hatua kubwa ya kupongezwa katika kuimarisha elimu ya mtoto wa kike hapa nchini.
Chilumba alisema,licha ya mafanikio hayo lakini bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya masomo ya Kompyuta Sayansi(ICT)uhaba wa viwanja vya michezo,ukosefu wa uzio,vitabu vya kiada na ziada kwa tahasusi zote,upungufu wa Walimu na vifaa vya kuhifadhia maji.
Awali katika risala ya Wanafunzi iliyosomwa na Stella Magaho walisema,walianza safari yao ya masomo mwaka 2023 kama wanafunzi wa kwanza wa kidato cha tano wakiwa jumla ya 210 na sasa wanaotarajia kuhitimu ni 204.
Magaho alisema,katika muda wa miaka miwili waliokuwepo shuleni wamepata mafanikio ya kitaaluma na kupata ujuzi kutoka kwa walimu ambao utawasaidia katika kujibu mitihani yao na kushiriki na kufanya midahalo mingi jambo ambalo limewasaidia kukuza uwezo wao hasa katika lugha ya Kiingereza.