Singida
Katibu wa Jumuiya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Singida Bi. Naomi Daudi ameipongeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa ujenzi wa barabara na madaraja kwa kutumia teknolojia ya mawe.
Bi. Naomi ameyasema hayo mara baada ya kutembelea banda la TARURA kwenye maonesho ya maadhimisho ya Kitaifa ya Usalama na Afya mahali pa kazi yanayoendelea kwenye Uwanja wa Mandewa mkoani Singida.
“Kilichonifurahisha hapa ni kwamba sasa tumeweza kuhamia kwenye teknolojia ya mawe na matofari ya kuchoma ambapo inakuwa kwa gharama ndogo”.
Amesema ubunifu huo wa watendaji wa TARURA itasaidia serikali kupunguza gharama na miradi mingi kutekelezwa kwa wakati.
Hata hivyo ameipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya TARURA katika kipindi chake na hivyo kuongeza ufanisi wa kazi na kusaidia kufungua barabara mpya nyingi na kujengwa kwa madaraja na vivuko vingi nchini.
Naye , Fundi Sanifu Mwandamizi wa TARURA wilaya ya Singida Bw. Felix Mwaituka amesema kwamba matumizi ya teknolojia hiyo yameweza kupunguza gharama kwa kiasi kikubwa.