Na Silivia Amandius.
Bukoba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Bi Fatina Hussein Laay, amefungua rasmi kikao kazi cha kudhibiti magendo ya kahawa leo, Aprili 28, 2025, katika ukumbi wa makao makuu ya Halmashauri.
Akihutubia kikao hicho, Bi Fatina amewataka maafisa kilimo kuhakikisha kuwa wakulima wanauza kahawa kwa wanunuzi wenye leseni pekee. Aidha, aliwataka wasimamie kwa karibu kuhakikisha wakulima wanauza kahawa iliyokomaa na kuonya dhidi ya kukausha kahawa kwenye udongo, akisisitiza kuwa kitendo hicho kinashusha ubora wa zao hilo.
“Nendeni mkadhibiti wafanyabiashara wanaopita kwa wakulima na kununua kahawa kwa kutumia vidumu bila kufuata mfumo rasmi wa ununuzi,” alisisitiza Bi Fatina.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kilimo na Uvuvi, Dkt. Kisanga Makigo, aliwahimiza maafisa kilimo kuhakikisha usajili wa mbolea katika mifumo rasmi, kufuatilia upimaji wa afya ya udongo, na kuhamasisha wakulima kushiriki katika chanjo za kitaifa kama vile chanjo dhidi ya homa ya mapafu na kideri cha kuku.
Washiriki wa kikao hicho, ambao ni maafisa kilimo kutoka maeneo mbalimbali, walitoa maoni yao na kuomba Serikali kuimarisha doria katika kipindi cha uvunaji na uuzaji wa kahawa ili kudhibiti magendo. Vilevile, walipendekeza kuongezewa vyombo vya usafiri kama pikipiki ili kuongeza ufanisi wa shughuli za ufuatiliaji wa kilimo mashinani.