*Mradi wa ujenzi wa mgodi kugharimu Trillioni 1.4
*Dhahabu ya kwanza kuanza kuzalishwa robo ya kwanza ya Mwaka 2027
*Rais Samia apongezwa kwa mazingira bora ya uwekezaji
*Mgodi kuzalisha Ajira na mapato kwa serikali
Kampuni ya Perseus ya Nchini Australia yatoa tangazo rasmi la kuanza ujenzi wa mgodi wa dhahabu wa Nyanzaga uliopo Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza.
Taarifa hiyo iliyotolewa leo tarehe 28 Aprili, 2025 imeeleza kuwa takribani kiasi cha Shilingi Trilioni 1.4 sawa na Dola za Kimarekani Milioni 523 (pamoja na dharura) zitawekezwa kujenga mgodi mkubwa unaotarajiwa kuzalisha dhahabu ya kwanza katika robo ya kwanza ya Mwaka 2027.
“Fedha zote za kujenga mgodi zitafadhiliwa na Perseus kupitia mikopo isiyo na riba, ambayo itapelekwa kwenye mradi wa Nyanzaga moja kwa moja. Na fedha hizo zote zipo kwani Perseus ina salio la pesa taslimu na bullion la dola za Marekani milioni 801 kufikia tarehe 31 Machi 2025” ilifafanua taarifa hiyo.
Kwa kutarajia maamuzi ya mwisho ya kuwekeza (Final Investment Decision – FID) katika mradi huo yangepitishwa na uongozi wa juu wa Kampuni ya Perseus, tayari Perseus imetumia takriban dola za Marekani milioni 27.5 katika kutekeleza shughuli za awali za maandalizi ya uwekezaji.
Shughuli hizo za awali za kujenga mradi wa Nyanzaga zilizokuwa zinaendelea ni pamoja na kama kuanzisha eneo la kufanyia kazi (site establishment), _earthworks_ , ujenzi wa kempu pamoja na kutekeleza Mpango wa Utekelezaji wa Uhamisho (RAP) na kujenga makao mapya kwa watu walioathiriwa na mradi.
Mara baada ya kutoka kwa tangazo hilo la Perseus, Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde (Mb) amesema taarifa hiyo ni njema kwenye kukuza sekta ya madini na ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo imeweka mazingira mazuri yanayoendelea kuvutia uwekezaji mkubwa nchini.
Vilevile, Mheshimiwa Mavunde alibainisha kwamba kutolewa kwa tangazo hilo na Kampuni ya Perseus kumeleta matumaini makubwa na kukata kiu ya wananchi wa Sengerema ambao wameusubiri mradi huo kwa muda mrefu na sasa ndoto yao inakwenda kutimia kwa kuona mradi mkubwa wa kuzalisha dhahabu unaanza ambao utasaidia upatikanaji wa mapato ya serikali,Ajira kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya Wilaya ya Sengerema na nchi kwa ujumla.
Aidha, Waziri Mavunde amesisitiza kwamba Wizara itaendelea kutoa ushirikiano kwa wadau wote wenye nia ya kuwekeza kwenye sekta ya madini nchini ili kufanikisha adhma yao na kupelekea kukuza uchumi wa Nchi na wananchi kwa ujumla.