Na Diana Byera, Misenyi.
MCHUNGAJI wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Kaskazini Magharibi (KKKT) Mtaa wa Mashasha wilayani Misenyi i Wilson Wilibadi amesema kuwa ataungana na waumini wake kuiunga mkono kwa vitendo Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia.
Aliyasema hayo mara baada ya timu ya wataalamu wanaoratibu kampeini hiyo katika wilaya hiyo kuungana na waumini wa Kanisa hilo kutoa elimu na ufafanuzi wa kisheria kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Sheria na jinsi ya kuyatatua
Mchungaji Wilibadi amesema ameifuatilia kampeni hiyo kupitia vyombo vya habari nchini na anapongeza ubunifu wa Serikali ya Mama Samia kwa kuwafikia wananchi wa pembezoni ambao hasa matatizo yao makubwa ni upungufu wa Sheria na elimu hiyo wanayoipata kupitia kwa wataalamu wa sheria anaamini itawasaidia kutoka sehemu moja hadi nyingine.
“Kwajinsi ambavyo nimefurahishwa na mafunzo ya kisheria nitaandaa kongamano kubwa la wanawake wa Kanisa hili na kuwaalika timu hii ya watalaam ili watoe mafunzo kuhusu haki zao kisheria ,jinsi ya kumiliki aridhi ,jinsi ya kupata mali zao hasa wajane na namna ya kukomesha ukatili kwani wanawake ndio waathirika wakubwa.”
Amesisitiza ni neema kubwa elimu hiyo kuwafikia kanisani na imethibitisha Serikali haina ubaguzi na amejifunza mambo makubwa aliyokuwa hayaelewi lakini baada ya kupata elimu amekuwa na ufahamu wa kutosha.
“Watalaam waliokuja kutoa mafunzo wamepikwa na kupikika ,nimefurahishwa sana na Mungu ampe nguvu Rais Dk.Samia Suluhu Hassan na aendelee kuwa mbunifu,”amesema Mchungaji Wilibadi
Mmoja wa waumini wa kanisa hilo ambaye ni mlezi wa mitaa ya washirika Winifirida Gabriel amepongeza elimu hiyo kutolewa kwa uwazi na kutoa nafasi ya wananchi kuuliza maswali na kujibiwa.
Ameiomba kampeni hiyo kuendelea kuwa endelevu hata ngazi ya vitongoji ili kupunguza kero na upotevu wa muda wa kupanga foleni mahakani na kudai kuwa kama wananchi watazijua vizuri Sheria watapunguza kuzivunja na kujiletea maendeleo .
Mafunzo ya masuala ya kisheria yaliongozwa na Mratibu wa kampeini hiyo Maximilian Fransis aliyekuwa na timu ya kampeni iliyotoa elimu kuhusu kuandaa wosia kisheria,mirathi,ukatilii,aridhi na masuala mengine ya kisheria huku waumini wa Kanisa hilo wakipewa nafa kuuliza maswali pamoja na kuwasilisha changamoto zinazowakabili ambazo zinahusu sheria.
Kampeni ya Mama Samia ilizinduliwa na Waziri wa Katiba na Sheria DK.Damas Ndumbaro mkoani Kagera Aprili 14 na mpaka sasa katika Wilaya ya Misenyi Kata 15 zimefikiwa.