Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete akipata maelezo ya matumizi ya gesi asilia kwenye magari kutoka kwa Mhandisi Nachael Mwanga pindi alipotembelea banda la GASCO.
Katika kuadhimisha Wiki ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi kitaifa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete ametembelea banda la Kampuni ya GASCO lililopo katika viwanja vya maonyesho mkoani Singida.
Waziri Ridhiwani alipata maelezo ya kina kuhusu hatua mbalimbali zinazochukuliwa na GASCO kuhakikisha usalama wa wafanyakazi na mazingira katika shughuli za uzalishaji na uendelezaji wa gesi asilia nchini. Maelezo hayo yalijumuisha mifumo ya usimamizi wa afya na usalama kazini, matumizi ya vifaa vya kisasa vya kujikinga, na hatua za dharura wanazozifuata endapo hali ya hatari itajitokeza.
Katika mazungumzo yake na maafisa wa GASCO, Mhe. Ridhiwani alipongeza juhudi za kampuni hiyo katika kuweka usalama wa wafanyakazi kuwa kipaumbele cha juu. Alisisitiza kuwa maendeleo ya sekta ya gesi asilia yanahitaji kuambatana na viwango bora vya usalama na mazingira ili kulinda rasilimali watu na mazingira ya nchi kwa ujumla.
‘‘Nafurahishwa kuona GASCO wakizingatia viwango vya kimataifa katika shughuli zao,” alisema Waziri Ridhiwani.
Wiki ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi huadhimishwa kila mwaka kama sehemu ya jitihada za serikali na wadau mbalimbali katika kuhamasisha umuhimu wa kuhakikisha kwamba maeneo ya kazi yanakuwa salama, yenye mazingira bora ya afya, na rafiki kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wao, maafisa wa GASCO walielezea dhamira ya kampuni hiyo ya kuendelea kuboresha mifumo ya usalama ili kuchangia maendeleo endelevu ya sekta ya nishati nchini Tanzania.