Na Janeth Raphael MichuziTv – Bubgeni -Dodoma
KATIKA kipindi cha mwaka mmoja, uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyounganishwa katika mfumo wa Gridi ya Taifa umeongezeka na kufikia MW 4,031.71 Aprili 2025.
Hayo yameelezwa leo Aprili 28,2025 Bungeni na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Dkt Doto Biteko wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
DKt Biteko amesema kutokana na jitihada zinazotekelezwa na Serikali katika kuimarisha uzalishaji wa umeme nchini kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali, Tanzania imeendelea kushuhudia ongezeko kubwa la uzalishaji wa umeme.
Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja, uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyounganishwa katika mfumo wa Gridi ya Taifa umeongezeka na kufikia MW 4,031.71 Aprili 2025,sawa na ongezeko la asilimia 86.6 ikilinganishwa na Megawati 2,138 zilizokuwepo mwezi Machi, 2024.
Aidha, kutokana na Serikali ya Awamu ya Sita kuendelea kuweka kipaumbele na msukumo madhubuti katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na umeme wa kutosha na uhakika, kumekuwepo na ongezeko kubwa la uzalishaji wa umeme katika mfumo wa Gridi ya Taifa tangu Mwaka 2020/21.
Dkt Biteko amesema mwaka 2020/21 uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyounganishwa katika mfumo wa Gridi ya Taifa ulikuwa ni MW 1,601.84, kwa sasa mitambo iliyopo ina uwezo wa kufua umeme wa MW 4,031.71, sawa na ongezeko la asilimia 151.7.
Aidha, hadi kufikia mwezi Aprili, 2025, mitambo ya kuzalisha umeme ambayo haijaungwa katika Gridi ya Taifa ina uwezo wa jumla ya MW 328.17 ambayo inajumuisha mitambo inayomilikiwa na TANESCO yenye uwezo wa kuzalisha MW 20.19 na MW 307.98 zinazozalishwa na kampuni binafsi kwa ajili ya matumizi ya kampuni hizo.
“Ni vyema kutambua kuwa kutokana na jitihada hizi, nchi yetu imeweza sasa kuondokana na mgao wa umeme ambao ulikuwa changamoto kubwa katika kipindi cha miaka mingi na kuwa na ziada ya umeme,”amesema Biteko
Aidha, kupatikana kwa umeme wa uhakika kumewezesha kupunguza gharama za uzalishaji na kufanya biashara nchini, kuzimwa kwa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta ambayo uendeshaji wake ni wa gharama kubwa.
“Na kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika vijijini, katika uendeshaji wa treni ya kisasa ya SGR na katika mikoa ambayo ilikuwa haijaungwa katika gridi ya Taifa.
Pia, upatikanaji huo wa umeme wa uhakika umechangia kukua kwa Pato la Taifa na kukabiliana na mfumuko wa bei kutokana na athari chanya za upatikanaji wa umeme huo katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na upatikanaji wa huduma.