Na Janeth Raphael MichuziTv -Bungeni -Dodoma
WIZARA ya Nishati imetaja vipaumbele vyake kwa Mwaka wa fedha 2025/26 ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Hayo yameelezwa leo April 28,2025 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Dkt Doto Biteko wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025- 2026.
Dkt Biteko amesema Wizara hiyo itaendelea kuimarisha uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, ikiwa ni pamoja na kufikisha Gridi ya Taifa katika mikoa iliyosalia ya Rukwa, Kagera, Lindi na Mtwara.
Aidha, Wizara itaanza utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Nishati wa Mwaka 2025 – 2030 (National Energy Compact 2025 – 2030).
Pia, upatikanaji na uunganishaji wa umeme kwa wananchi, kuongeza mchango wa nishati jadidifu katika uzalishaji wa umeme na ushiriki wa Sekta Binafsi katika maendeleo ya Sekta ya Nishati.
Vilevile, Wizara itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kutekeleza Mradi wa Kuimarisha Gridi ya Taifa (National Grid Stabilization Project) pamoja na kufanya matengenezo na ukarabati wa mitambo ya kuzalisha umeme.
Dkt Biteko ameyataja maeneo mengine ya kipaumbele ni kuendelea na usambazaji wa nishati katika vitongoji, maeneo ya migodi, kilimo, viwanda na pampu za maji pamoja na vituo vya afya ili kuwezesha shughuli za uzalishaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi; pamoja na kuhamasisha na kuwezesha watanzania kutumia nishati safi ya kupikia.
“Ikiwa ni utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) na Mpango wa Taifa wa Nishati wa Mwaka 2025 – 2030,”amesema Naibu Waziri Mkuu.
Vilevile,Wizara pia itaendelea kuwezesha upatikanaji wa bidhaa za mafuta vijijini kupitia ujenzi wa vituo vya mafuta katika maeneo hayo; pamoja na kutekeleza shughuli za utafutaji,uendelezaji na usambazaji wa mafuta na gesi asilia na kutekeleza miradi ya kielelezo.
“Na kimkakati ya mafuta na gesi asilia ikiwemo Mnazi Bay Kaskazini, Eyasi Wembere, mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia kuwa Kimiminika (Liquefied Natural Gas LNG Project) na ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania (East African Crude Oil Pipeline – EACOP),”amesema Naibu Waziri Mkuu Biteko
Dkt Biteko amesema Jitihada zitaelekezwa pia katika kusimamia na kuhakikisha nchi inakuwa na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa za mafuta ya petroli pamoja kuimarisha matumizi ya gesi asilia (CNG) katika vyombo vya moto.
Vilevile, Wizara itaendelea kutekeleza shughuli za kiudhibiti; kuimarisha ushiriki wa wazawa katika Sekta ya Nishati pamoja na kuimarisha nguvu kazi na kuwezesha upatikanaji wa vitendea kazi ili kuimarisha tija na ufanisi katika utendaji kazi.
Pia, Wizara itaendelea kuimarisha utendaji wa Taasisi/Mashirika yaliyo chini yake ya TANESCO, REA, TPDC, PBPA, EWURA na PURA pamoja na Kampuni Tanzu ili yaweze kuimarika zaidi katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi pamoja na tija na ufanisi katika utendaji.