NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt.Mohamed Said Dimwa,akizungumza na wajumbe wa kamati za siasa za Matawi,Wadi,Majimbo na Wilaya ya Mkoani Kichama,katika ziara ya Sekretarieti ya Kamati Maalum ya NEC,CCM Taifa Zanzibar.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt.Mohamed Said Dimwa, akijadiliana na mjumbe wa kikao hicho juu ya masuala ya utendaji wa Chama na Jumuiya.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt.Mohamed Said Dimwa,akikagua gwaride la Vijana wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba,baada ya kuwasili mkoani humo kwa ajili ya ziara ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi.
……
NA MWANDISHI WETU, PEMBA.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt.Mohamed Said Dimwa, amesema Chama hicho kimejipanga kuhakikisha kinashinda majimbo yote ya Pemba,kutokana na wananchi wa kisiwa hicho kukiri kuwa CCM imeisimamia vizuri Serikali yake katika kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa kijamii.
Hayo ameyasema wakati akizungumza na wajumbe wa Kamati za siasa za Matawi,Wadi,Majimbo ya Wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba katika ziara ya Sekretarieti ya Kamati maalum ya NEC,CCM Taifa Zanzibar iliwa ni mwendelezo wa ziara za kuimarisha uhai wa CCM kuelekea uchaguzi mkuu wa Octoba 2025.
Alieleza kuwa maelfu ya waliokuwa Wanachama wa ACT-Wazalendo wakiwemo vigogo,makada na wanachama wa miaka mingi wameendelea kujiunga na CCM huku wakieleza kuridhishwa na sera za Chama Cha Mapinduzi hatua inayoongeza uhalali wa ushindi katika uchaguzi ujao.
Alisema ushindi huo utapatikana kupitia uchaguzi huru,haki na wa demokrasia na kwamba utang’oa mizizi yote ya upinzani hasa ACT-Wazalendo ili kuendeleza safari ya kuifungua kiuchumi baada ya ushindi huo kuelekea 2030.
Dkt.Dimwa ambaye pia Mwenyekiti wa Sekretarieti hiyo amefafanu kwamba, miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika sekta na Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi ni suluhu ya kumaliza changamoto za wananchi.
Alitaja moja ya sababu ya CCM kushinda kuwa ni mwitikio wa wanachama wake waliojiandikisha kwa wingi katika daftari la wapiga kura,sambamba na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi uliomaliza changamoto za wananchi wa mijini na vijijini kwa zaidi ya asilimia 98.
Kupitia Mkutano huo Dkt.Dimwa, aliwambia wajumbe hao kuwa CCM itawasimamisha kazi na wengine kuwapeleka katika Kamati za usalama na maadili watendaji na viongozi wake watakaojihusisha na vitendo vya kuhujumu mchakato wa uchaguzi wa ndani wa kura za maoni za kupata wagombea wa nafasi za Ubunge,Uwakilishi na Udiwani.
Alisema CCM itaanza kufanya usafi wa ndani kwa kuchukua hatua za kinidhamu kwa baadhi ya watendaji wake wanaofanya udalali wa kisiasa kwa maslahi yao binafsi na wengine kutumiwa na baadhi ya watu wagombea (watia nia) kuvunja taratibu na miongozo ya CCM kwa ajili ya maslahi binafsi yasiyo na tija kwa Chama na jumuiya.
Dkt Dimwa,ameeleza kwa uwazi kuwa fagio Hilo litakuwa ni maandalizi ya kuhakikisha wanapatikana viongozi bora wasiokuwa na chembechembe za rushwa,udalali wa kisiasa ndani ya Chama na jumuiya zake na viongozi wenye utu na uzalendo wa kusimamia na leta maendeleo ya wananchi wote.
Katika maelezo yake Dkt Dimwa,amesema anatumia ziara hiyo kutoa onyo kwa wote walioanza kupitia wagombea na kubeba mikoba yao kabla ya Chama Cha Mapinduzi kutoa ruhusa ya kuanza kwa kampeni,kuhakikisha wanaacha tabia hizo na kuheshimu utaratibu uliowekwa.
Alisema kupitia kikao cha Mkutano Mkuu maalum wa CCM uliofanyika 18-19 Januari,mwaka 2025 kimefanya mabadiliko ya Katina yake ya 1977 toleo la 2022 kwa kuongeza idadi ya wapiga kura katika mchakato wa ndani wa kura za maoni ili kuongeza upana wa uwazi,uhuru na demokrasia ndani ya Chama.
“Natumia ziara hii kutoa onyo kwa watendaji wote na viongozi waliopo katika usimamizi ya Chama kuacha tabia ya kutumiwa na watu kuharibu utaratibu na kanuni za Chama,,,,hatuwezi kuacha vitendo hivi viendelee tunataka kupata wagombea safi watakaouzika na kukubalika uchaguzi ujao.
Lazima Chama kirudi kwa wanachama wenyewe,hiki sio Chama Cha wapiga deal (wababaishaji) bali ni Chama Cha kijamaa yaani wakwezi,wakulima na wafanyakazi ni lazima tulinde misingi ya ASP na TANU.”alisema Dkt.Dimwa.
Alisema lengo la ziara hiyo ni kuimarisha Chama iliwa ni sehemu ya kufanya mambo tisa (9) muhimu ya kuelekea katika uchaguzi mkuu yakiwemo kuepuka rushwa pamoja na wanachama kujitokeza kugombea katika uchaguzi wa ndani wa kura za maoni.
Aliendelea kuyata mambo hayo kuwa ni pamoja na wanachama na wananchi kuipigia kura CCM ishinde kwa kushindo 2025,umuhimu wa makundi maalum kushiriki kuwania uongozi,kuacha kuchafuana kisiasa,ulipaji wa ada,uchaguzi wa kidemokradia wa kura za maoni pamoja na utekelezaji wa ibara ya 5 katika uchaguzi mkuu inayotaka Chama kishinde kwa ngazi zote.
Mjumbe wa Sekretarieti ya Kamati maalum ya NEC,CCM Taifa Zanzibar ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Abdi Mahmoud Abdi,alisema kundi la vijana wa Chama hicho wanatakiwa kuwa mfano bora wa kukipigania Chama Cha Mapinduzi kuhakikisha kinashinda na wanapatika viongozi bora wenye uwezo wa kuleta maendeleo endelevu kwa jamii.
Akizungumza Mjumbe wa Sekretarieti ya Kamati maalum ya NEC,CCM Taifa Zanzibar ambaye pia ni Katibu wa Kamati maalum ya NEC,idara ya organazesheni CCM Zanzibar Ibrahim Omar Kilupi,aliwasihi wajumbe hao kufanya maamuzi sahihi ya kuhakikisha wagombea wote wanaowateua katika kura za maoni wanakuwa ni wazuri na watakaouzika na kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu wa Octoba 2025.
Kilupi,amesema CCM imejipanga vizuri kuendelea kufanya siasa za kistaarabu zinazozingatia ushindani huru unaozingatia matakwa ya Demokrasia.
Naye Mjumbe wa Sekretarieti ya Kamati maalum ya NEC,CCM Taifa Zanzibar Yahya Abdalla Rashid,amesema kazi kubwa aliyobaki kwa Sasa ni kuendelea kuhamasishana baina ya wanachama na wananchi kuhakikisha wanawapigia kura nyingi wagombea wote wa CCM katika uchaguzi mkuu wa Octoba 2025.
Kwa upande wake Mjumbe wa Sekretarieti hiyo ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa U.W.T Zanzibar Tunu Juma Kondo,aliwasisitiza wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea katika kura za maoni za uchaguzi wa ndani kwa nafasi za ubunge,uwakilishi na udiwani ili waweze kushika uongozi katika vyombo vya maamuzi.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba Yussuf Ali Juma,amesema mkoa huo umeendelea kupiga hatua kubwa za kimaendeleo kutokana na juhudi kubwa za utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 katika sekta mbalimbali zikiwemo ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya barabara, maji,ukarabati wa bandari ya mkoani,Hospitali za kisasa,vituo vya afya vyenye vifaa tiba na madaktari,uwezeshaji wa makundi ya ujasiriamali kwa vijana na wanawake pamoja na Serikali kupunguza Kodi za usafirishaji wa bidhaa za vyakula kisiwani Pemba.
Alisema wanachama na wananchi kwa ujumla katika mkoa huo wanawapongeza kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi kwa kutekeleza kwa ufanisi ahadi za maendeleo zilizoahidiwa kupitia kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.