Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa vitabu 760 kwaajili ya wanafunzi wa kidato vha tano na sita kwa Shule ya Sekondari ya Ingwe iliyopo wilayani Tarime mkoani Mara lengo likiwa ni kuboresha taaluma shuleni hapo.
Rais Samia ametoa vitabu hivyo baada ya kupokea ombi la Mkuu wa Mkoa wa Mara aliloliwasilisha kwake wiki mbili zilizopita kuhusu changamoto ya upungufu mkubwa uliokuwa ukiikabili shule hiyo hivyo kurudisha nyuma jitihada za serikali za kuboresha huduma za kijamii ikiwepo elimu.
Akipokea vitabu hivyo ambavyo baadhi ni vya masomo ya jiografia,historia, kiswahili na kingereza,Mkuu wa Shule hiyo, Elika Mbeleyesimu amesema vitabu hivyo vimemaliza kabisa changamoto ya upungufu wa vitabu iliyokuwa ikiikabili shule hiyo kwa wanafunzi hao wa kidato cha tano na sita.
“Vitabu hivi vitatusaidia kuboresha taaluma shuleni hapa hasa katika kampeni yetu ya kutokomeza daraja la pili kwa mtihani wa taifa wa kidato cha sita na kubaki na daraja la kwanza pekee, sasa kila mwanafunzi atakuwa na nafasi ya kutumia kitabu kwaajili ya kufanya rejea na mazoezi mengine,” amesema
Amesema vitabu hivyo vitawanufaisha wanafunzi wote 332 wa kidato cha tano na sita wanaosoma shuleni hapo.
Akikabidhi vitabu hivyo kwa niaba ya Mkuu wa mkoa, Mkuu wa wilaya ya Tarime, Edward Gowele amesema kutokana na unyeti wa suala hilo mkuu wa mkoa aliamua kufikisha changamoto hiyo kwa Rais Samia ili iweze kufanyiwa kazi kwa haraka na kupatiwa ufumbuzi.
“Tunamshukuru mkuu wa mkoa kwa kulichukua suala hili kwa unyeti na upekee wake hadi kufanikisha upatikanaji wa vitabu hivi ndani ya wiki mbili,sasa kazi kwenu wanafunzi someni kwa bidii sisi tunawadai matokeo mazuri tu,” amesema
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Lucia Nashon wa kidato cha tano amesema awali shule yao haikuwa na vitabu kwaajili ya wanafunzi badala yake vitabu vilivyokuwepo vilikuwa vikitumiwa na walimu pekee kwaajili ya kufundishia.
“Hapakuwa na vitabu kwaajili ya wanafunzi na vichache vilivyokuwepo vilikuwa vikitumiwa na walimu kwaajili ya kufundishia kwahiyo tulikuwa hatuna namna yoyote ya kufanya rejea wakati wa daarsani au hata tukiwa tunajisomea lakini kwa vitabu hivi changamoto hii sas ani historia,” amesema
Changamoto ya ukosefu wa vitabu shuleni hapo liliibuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi aliyefanya ziara shuleni hapo wiki mbili zilizopita ikiwa ni sehemu ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Kanali Mtambi alifanya ziara shuleni hapo Aprili 14,2025 na kuwataka wanafunzi kueleza changamoto walizokuwa nazo ambapo pamoja na mambo mengine wanafunzi hao walieleza kuhusu ukosefu wa vitabu shuleni.
Kutokana na changamoto hiyo,Mkuu huyo wa mkoa aliahidi kufanyia kazi suala hilo huku akisema ni vigumu kupata matokeo chanya endapo shule inakabiliwa na ukosefu wa vitabu kama ilivyokuwa kwa shule hiyo.
“Hili suala nalichukua na kwenda kulifanyia kazi haraka iwezekanavyo kwani pamoja na mambo mengine uwepo wa vitabu vya kutosha shuleni kuna mchango kubwa sana wa kuboresha taaluma,” alisema Mtambi