Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda amehitimisha mafunzo ya Askari wapya katika Shule ya Mafunzo ya Awali ya Kijeshi iliyopo Kihangaiko, Msata Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani, leo tarehe 29 Aprili 2025.
Askari waliohitimu mafunzo wamekula kiapo cha utii mbele ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi.
Akizungumza wakati wa sherehe hizo, Mkuu wa Majeshi Jenerali Mkunda amewataka Askari wapya kwenda kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia kiapo cha utii, na kuwajibika kulinda mipaka ya nchi, kuilinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumtii Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu.
Askari wapya wametakiwa kutunza afya zao kwa kuwa muda wote wanatakiwa kuwa na utimamu wa afya ili waweze kulitumikia Taifa kama walivyokusudiwa.
Aidha, Jenerali Mkunda amewaasa Askari kuzingatia mambo manne kwa Mwanajeshi ambayo ni Nidhamu nzuri, Utii, Uhodari na Uaminifu kwani Taifa linawaamini na kuwategemea katika ulinzi.